NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 8:
Mara mlango wa Sam ukaanza kugongwa kwa nguvu sana hadi tukashtuka.
Sam akainuka na kutaka kwenda kufungua, nikamshikilia mkono kumzuia kuwa asiende.
"Mbona unanizuia Sabrina?"
"Usiende kufungua Sam"
"Kwanini? Kwani unamjua mgongaji wewe?"
Nikatikisa kichwa kwa kukataa kuwa simjui.
"Kama humjui kwanini hutaki niende kumfungulia?"
Nikawa namuangalia tu Sam bila ya kusema chochote huku jasho jingi likinitoka.
"Wewe Sabrina nadhani una matatizo wewe sio bure, niachie basi nikamfungulie"
"Muulize kwanza ni nani ndio nitakuachia"
Nilizidi kumshikilia Sam, akauliza kuwa anayegonga ni nani ila mgongaji hakujitaja jina na kuzidi kugonga tu. Mi nikazidi kuogopa na kumuangalia Sam,
"Si unaona hataji jina lake? Huyo si mwanadamu wa kawaida Sam"
"Unamaana gani?"
"Nimeota vibaya Sam na simuamini mgongaji"
"Acha mambo ya ajabu Sabrina, hakuna chochote kibaya. Acha tu nikamfungulie"
Nilizidi kumkataza Sam ila hakunisikia hata kidogo, akainuka na kwenda kufungua mlango ambapo nilijiziba sura ili nisiweze kushuhudia kinachotokea.
Mlango ulipofunguliwa tu, yule mgongaji aliingia moja kwa moja tena kwa mbwembwe na kelele nyingi.
"Surpliiiiiseeeeeeee..........."
Akaja na kunikumbatia, nikatoa mkono machoni alikuwa ni Lucy.
Nikashangaa sana, Lucy amefata nini kwa Sam na je amepajuaje? Sikuwa na furaha kabisa na kuwauliza.
"Mbona sielewi?"
Sam nae akajibu,
"Hata mi mwenyewe sielewi, ngoja Lucy atufafanulie mwenyewe"
Nikamuangalia Lucy kwa jicho kali sana.
"Umefata nini hapa Lucy? Nani amekuelekeza huku?"
"Punguza hasira mumy nikwambie"
"Haya niambie, nahitaji kueleweshwa"
"Kuna siku nilimuuliza Sam anapoishi nae akanielekeza, kwavile mitaa hii naijua wala haikunipa tabu kupafahamu hapa na nilimwambia kuwa ipo siku nitamtembelea. Leo asubuhi nilipozungumza nae akaniambia kuwa wewe unakuja kwake na mimi nimeona leo kuwa siku bora ya kuwasurplise"
Kwakweli maelezo ya Lucy sikuyapenda na wala tabia ya Lucy sikuipenda pia.
Rafiki gani huyu? Utafanyaje surplise kwa mpenzi wa mwenzio anakuhusu? Marafiki kama hawa ndio huusika kuharibu mahusiano ya watu.
Akaanza kufungua mzigo wake kuwa amebeba na keki na vinywaji ili tufurahie pamoja, sikujisikia kula chochote kile alichobeba Lucy hadi Sam akaniuliza.
"Mbona hivyo Sabrina wangu jamani? Punguza kisirani mama, mimi ni wako tu. Njoo tule pamoja"
Ingawa alinilainisha kwa maneno ila moyo wangu bado ulisita kula vitu alivyobeba Lucy.
"Sijisikii kula mpenzi, tumbo langu limejaa sana"
Sikutaka Sam aendelee kuniona kuwa nina kisirani, ila kula sikujaribu hata kidogo licha ya Sam kunilazimisha sana.
Sam na Lucy waliendelea kufurahia, maneno ya Lucy yakawa yananichefua.
"Susa mama sie twalaaa"
Yani nilitamani nimponde Lucy na hata Sam nae sijui alikuwaje kwani hakuweza kabisa kumfokea Lucy.
Baada ya kukata ile keki na kula kisha kunywa vile vinywaji, Lucy akaomba tufungulie mziki ili acheze.
Sam akainuka na kufungulia mziki, Lucy akawa anacheza huku akijibidua na kujishebedua, roho ilizidi kuniuma.
Sam akaniambia niinuke ili tucheze wote nikagoma, mara nikamsikia Lucy akisema.
"Kama hataki kucheza njoo ucheze nami Sam, nipo single hapa uuuhuuu"
Huku akizungusha kiuno chake, hasira zikanikamata na kuinuka, kwakweli uzalendo ulinishinda jamani. Nikaenda kuzima ule mziki, Lucy akawa wa kwanza kuuliza.
"Mbona umezima mziki Sabrina?"
"Tafadhari Lucy naomba tuheshimiane"
"Kwani kosa langu nini?"
"Kukutambulisha shemeji yako isiwe sababu ya wewe kujitawala kiasi hiko, unatamani kucheza mziki nenda disko kwanza hakuna aliyekuita hapa. Kama vipi jiondokee tu."
Sam akaingilia kati yale mazungumzo, nadhani na yeye alinogewa na kiuno cha Lucy jinsi kilivyokuwa kinazunguka.
"Punguza hasira Sabrina, sijaona kosa lolote alilofanya Lucy. Amekuja kutuchangamsha tu hapa."
"Unajua usinichanganye Sam! Kwanza wewe na Lucy mmejuana vipi kwa sura mpaka Lucy kuingia moja kwa moja ndani?"
"Sabrina mpenzi, Lucy nimemjua kupitia wewe na leo ndio mara yangu ya kwanza kumuona. Punguza hasira mama"
Hasira nilizokuwa nazo zilikuwa ni za hali ya juu na niliona Sam akinidanganya tu, kisha akamgeukia Lucy.
"Usijali shem, ipo siku tutapanga twende huko disko"
Lucy akawa amesimama tu kutuangalia, nikaona Sam nae ananizingua nikainuka na kubeba mkoba wangu ili niondoke mimi halafu yeye aendelee kufurahi na Lucy wake.
Kabla sijafungua mlango, Sam alikuja na kunizuia kuwa nisitoke.
Kisha Lucy akatoka mule ndani, Sam akaendelea kunishikilia mkono.
"Tafadhali Sabrina, usifanye hasira kama za siku ile nakuomba"
"Sam, niache niende"
"Siwezi kukuacha uende mwenyewe Sabrina, leo nitakupeleka mimi hadi nyumbani kwenu"
Lucy alikuwa ametoka ila amesimama palepale nje bila ya kwenda popote, ikabidi nimwangalie Lucy na kumwambia.
"Si uondoke, unachongoja hapo kitu gani?"
Lucy akatabasamu kisha akaondoka, nikabaki mimi na Sam sasa.
Sam aliendelea kunibembeleza kuwa nitulie, nami nikatulia kwa muda na kumwambia kuwa nataka kurudi nyumbani. Akaniomba kuwa niingie tena ndani ili na yeye ajiandae tutoke, nikarudi mule ndani kwa Sam.
Mezani nikaona pochi ya Lucy, eti Lucy alisahau ile pochi yake ndogo nikajua hayo ni majaribu tu na Lucy amefanya kusudi kuacha pochi ili aweze kurudi tena. Nikachukua simu na kumpigia, nikamwambia kuwa amesahau pochi yake ndogo akasema kuwa ameshafika mbali na atakuja kuichukua siku nyingine eti hawezi kurudi tena muda huo wakati ameondoka pale muda sio mrefu, nilichukia sana kwani Lucy anajiamulia tu kama mahali ni pake.
Nikamuangalia Sam na kumwambia,
"Kwahiyo hiyo pochi ndio itakuja kukuunganisha tena na Lucy?"
"Hapana Sabrina, unanifikiria vibaya tu."
Wazo lingine likanijia kuwa niichukue mimi ile pochi na kwenda nayo ili Lucy aikute kwetu ila moyo wangu ukasita, kwahiyo sikuichukua tena.
Niliondoka na Sam pale nyumbani kwake akinisindikiza nyumbani, njiani tulikuwa kama mabubu kwani sikutaka kuzungumza nae kabisa ingawa kuna muda alikuwa akijiongelesha mwenyewe tu bila ya kujibiwa. Mawazo yangu yalikuwa ni kwa Lucy jinsi alivyokuwa akikatika mbele ya Sam, tukapanda daladala ila sikukaa nae siti moja nilikaa na mkaka mwingine kabisa aliyeanza kuniongelesha kwa kunisifia.
"Una sura nzuri dada, nimevumilia nimeona nikwambie ukweli tu"
Na mimi nikacheka, ambapo nikampa upenyo wa kuongea maneno mengi zaidi.
"Mmh! Tabasamu lako limegusa hadi moyo wangu Sabrina"
Nikashtuka sana na kumuangalia kwa makini,
"Umejuaje jina langu?
"Aaah! Samahani, ulipokuwa chini nilimsikia jamaa yako akikuita Sabrina kuwa mpande hili gari"
Hapo kidogo nikapumua ingawa sikuwa na uhakika kama kweli Sam aliniita jina pale chini, yule mkaka akaendelea kujiongelesha.
"Naitwa Carlos na nimefurahi sana kufahamiana na wewe Sabrina, je naweza pata mawasiliano yako?"
Nikamuangalia Sam aliyekuwa amesimama kwakuwa yeye hakupata siti, macho yangu yakagongana na macho ya Sam akanikonyeza na kutabasamu nami nikainama chini kwa aibu.
Yule mkaka akaniongelesha tena,
"Naomba namba yako ya simu Sabrina"
Nikampa jibu la haraka hata bila ya kufikiri mara mbili,
"Sina simu"
"Sawa bhana Sabrina, milima haikutani lakini binadamu hukutana"
Tukafika kituoni na kushuka.
Sam akanisindikiza hadi nyumbani mlangoni kabisa, alihakikisha nimeingia ndani ndipo akaondoka.
Nilimkuta dada akijilalamisha ndani,
"Sijui mkaka wa watu akitokea tena kunidai yule mdoli wake nitafanyaje?"
"Hakuna la kufanya Penina, maji yakimwagika hayazoleki. Ukimuona mwambie ukweli tu huenda akaelewa.
Nikawasalimia pale na kwenda chumbani kwangu.
Baada ya kuoga na kula nilikaa nao pale sebleni ambapo baada ya muda wakainuka na kwenda kulala kwani ilikuwa ni usiku.
Nilikaa nikiwasiliana na Sam kwa njia ya ujumbe mfupi ila kichwani ilikuwa inanijia sura ya Carlos mkaka niliyekutana nae kwenye daladala.
Mara nikasikia kama vile kuna watu pale sebleni wakizungumza ila sielewi maneno yao wala wao hawaonekani. Nikaamua kwenda chumbani kwa uoga.
Nilipokuwa chumbani nikampigia simu Sam ili nijiliwaze kwanza.
Ila simu ya Sam ilikuwa inatumika, nikimtumia ujumbe anajibu ila simu yake ukipiga inatumika. Nikapatwa na wazo kuwa Sam anaongea na Lucy tu, nikajaribu kumpigia Lucy nae namba yake ilikuwa inatumika kwakweli nikaona Lucy anataka kuninyang'anya tonge mdomoni kabisa yani.
Nikawaza sana na usingizi kunichukua.
Nikamuona yule mkaka wa ndotoni akimkabidhi Lucy ile keki na juisi, halafu akaniangalia na kusema.
"Umekataa kabisa hata kuonja zawadi niliyokufungia Sabrina? Kila zawadi yangu huitaki ila najua kuwa ipo siku utakayopokea zawadi yangu kwa moyo mweupe na kuitumia, na hapo utakuwa wangu milele"
Akawa anatabasamu.
Nikashtuka gafla na jina la kwanza kunitoka mdomoni ni,
"Carlos"
Nikakaa ni kujiuliza kuwa kuna mahusiano gani na Carlos kijana niliyekutana nae kwenye daladala na huyu mwanaume wa ndoto zangu? Nikajiuliza maswali mengi na kukosa majibu, na je Lucy yeye anahusika vipi na huyu mkaka wa ndotoni.
Maneno ya yule mkaka kwenye daladala yalikuwa yakitembea akilini mwangu kuwa milima haikutani lakini binadamu hukutana.
Nilitamani nitoke chumbani ila zile sauti za sebleni zilinitisha.
Mara nikahisi kama vile kuna mtu anatembea tembea karibu na mlango wangu, uoga ulinishika nikajifunika sana shuka na kupitiwa na usingizi hadi kuna kucha.
Kesho yake sikutaka kupoteza muda, nilimpigia simu Suzy ili nipate kumueleza mambo aliyonitenda Lucy.
Nikiwa namngoja Suzy aje, nilimfata dada Penina na kumuuliza maswali yangu baadhi.
"Eti dada, mwanamke anayeweza kucheza sana mziki ndio anapata mchumba kiurahisi?"
Dada akacheka sana.
"Ingekuwa hivyo basi wale wanenguaji wa kwenye bendi wote wangekuwa wameshaolewa. Kucheza muziki sio kumridhisha mume, zipo njia za kumfanya mwanaume afurahi kuwa na wewe."
"Njia zipi hizo?"
"Maswali mengine kamuulize mamako huko anatamani kweli kuulizwa maswali hayo."
Mama akasikia na kuuliza,
"Maswali gani tena?"
"Mwanao anataka kujua njia za kumridhisha mume"
Halafu akacheka, mama akaniita.
"Sabrina mwanangu mbona unapenda kuharakia mambo? Muda ukifika utaambiwa yote."
"Ila mama sidhani kama kuna ubaya nikijua hata kidogo."
"Ameshaanza kukuchanganya huyo Sam mwanangu, maana wewe hata husikii unachoambiwa. Nitakufundisha siku ukija kumtambulisha mwanaume mwingine tofauti na Sam hapa nyumbani kwangu.
Ikabidi nitulie kumngoja Suzy afike nyumbani.
Suzy alipofika nikamsimulia jinsi Lucy alivyofanya nyumbani kwa Sam na vile alivyoacha pochi yake.
"Shoga yangu, ukicheka na nyani utavuna mabua. Nilishakwambia kama Lucy si mtu mzuri ila wewe unamchekea tu, shauri yako"
"Sasa nifanye nini jamani Suzy?
"Kwanza umekosea sana kuiacha pochi ya Lucy nyumbani kwa Sam, hujui kama unampa nafasi ya kujitawala? Bora ungeondoka nayo mwenyewe"
Hapo hapo nikaona kuwa itakuwa ni vyema kama tukifata ile pochi kwa Sam kabla Lucy hajaenda ili nimpigie simu na kumwambia kuwa aifate nyumbani kwetu.
Suzy akanisaidia kuaga kwa mama ila hatukusema kama tunaenda kwa Sam.
Safari ikawa moja kwa moja kwa Sam, na ile kufika tu, kwa mbali nikamuona mtu kama Lucy akitoka mule ndani kwa Sam huku jasho likimtoka.
Nikamuacha Suzy akiwa kaduwaa pale nje nami nikakimbilia chumbani kwa Sam ili kumuona Sam ana hali gani.
Nikamkuta Sam amelala kitandani ila akiwa hajitambui kabisa, ikabidi nimuite Suzy ili aje kusaidiana nami mule ndani na tujue Sam kapatwa na tatizo gani.
Ila hakuingia Suzy kama nilivyotarajia, bali aliingia mkaka. Kumuangalia ni yule Carlos wa kwenye daladala.
Itaendelea kesho.....!!!
Asanteni kwa maoni yenu wadau.
Kama tuko pamoja
![]()
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:
Post a Comment