Social Icons

Monday, 19 June 2017

HADITHI: Niliolewa na Jini bila ya kutarajia - 9


NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 9:

Ila hakuingia Suzy kama nilivyotarajia, bali aliingia mkaka. Kumuangalia ni yule Carlos wa kwenye daladala.
Nikashtuka sana na kuanza kutetemeka kwa uoga, nikainuka na kujibanza ukutani kama vile nauomba ukuta ufunguke nitoke nje mara Suzy akaingia nyuma yake na kusema.


"Nimeona mkaka huyo anapita, kwajinsi ulivyoniita kwa nguvu nikajua lazima kuna matatizo ndio nikamuomba atusaidie. Mbona umejibanza ukutani sasa?"
Nikawa kama mtu aliyetoka ndotoni, nikamuangalia yule kaka ambaye alikuwa akiniangalia na mimi.
"Wewe si Carlos wewe?


"Ndio mimi ni Carlos kwani kuna tatizo?"
"Hapana, si tulikutana kwenye daladala jana?"
"Ndio tulikutana Sabrina, hata hivyo milima haikutani binadamu hukutana. Tumsaidie mwenzetu kwanza.


Akainama na kumnyanyua Sam, ila bado sikupenda kusaidiwa na yule Carlos ingawa tulifatana nae hadi kwenye gari ambayo ilikuwa kama inatungoja sisi.
Sam akawekwa kiti cha nyuma ambapo nilikaa nae halafu Suzy na yule mkaka walikaa siti za mbele, gari ikaanza kuondoka huku yule mkaka akidai kuwa tunaenda hospitali.


Kufika njiani, Sam akazinduka ambapo alidai kuwa kichwa kinamuuma sana na hata hakuweza kuongea zaidi. Yule mkaka akasimamisha gari na kusema kuwa tumnunulie dawa ya kutuliza maumivu ya kichwa kwanza kabla ya kufika hospitali, kwakweli hata sikujua alikuwa na lengo la kutupeleka hospitali gani.


Gari ikasimama karibu na duka la madawa, Suzy akashuka na kununua dawa na maji kisha tukampa Sam anywe. Alipokunywa tu akasema kuwa amepona na kichwa hakimuumi tena na akachangamka sana kupita maelezo huwezi hata kusema kuwa alianguka, yule mkaka akageuka na kutuuliza.
"Kuna haja ya kwenda hospitali tena?


Sam akajibu tena kwa uchangamfu wa hali ya juu,
"Hakuna haja, kama aliyekuwa anapelekwa hospitali ni mimi basi hakuna haja maana nimeshapona kabisa"
Nikamuangalia Sam kwa makini.


"Usiseme haina haja Sam, tumekukuta na hali mbaya sana unatakiwa ukapime. Kwani nini kilikupata?"
"Hata sijui kilichonipata."
"Kama hujui basi inabidi twende hospitali ili tujue nini tatizo."
"Haina haja bhana.


Nikaona kama nachezewa mchezo tu hapa yani Sam tuliyemkuta hoi hajitambui kabisa eti saa hizi anakataa kwenda hospitali, nikajua lazima kuna kitu kimejificha. Swali jingine likanijia kuwa yule Lucy aliyekuwa anatoka chumbani kwa Sam muda ule huku akitokwa na jasho alikuwa ametoka kufanya nini.


"Na Lucy alivyotoka chumbani kwao, mlikuwa mnafanya nini au alikufanya nini?"
Sam akajifanya kushangaa,
"Lucy!! Sijamuona Lucy ndani kwangu mimi"
"Eti Suzy hukumuona yule mdada aliyetoka kwenye chumba cha Sam?


"Mmh! Sikumuona mtu kwakweli ila nilishangaa kukuona wewe ukikimbilia lile eneo la tukio"
Hapa ndipo walipozidi kunichanganya jamani, baada ya Sam kukataa kwenda hospitali yule mkaka aligeuza gari na kuturudisha kwa Sam.


"Jamani, nadhani huu ndio mwanzo mzuri wa kufahamiana. Mimi naitwa Carlos na nyie wenzangu nimewasikia majina yenu mkiitana, kuwa huyu Suzy na huyu Sam na Sabrina. Naona S zimetawala hapo.


Sam akacheka na kumwambia Carlos,
"Hata wewe ni mwenzetu, naona una S mwishoni mwa jina lako"
Wakafurahi wote kasoro mimi niliyekuwa na mawazo bado.


Tukaingia ndani wote na wala yule Carlos hakuondoka, bado nikaendelea kujiuliza yani huyu mkaka kutoa msaada ndio anazamia moja kwa moja! Inamaana hana mambo ya kufanya?
Nadhani alicheza na mawazo yangu na kuamua kuaga, kisha akamuomba Sam namba ya simu alipopatiwa akaondoka.


Nikaangalia kwenye meza ya Sam na kuona kuwa pochi ya Lucy bado ipo, nikamwambia Suzy.
"Pochi yenyewe ya Lucy hiyo hapo"
"Mpigie simu aje kuifata hata wakati tupo wote, na ilete tuione"
Nikampigia Lucy simu aje na wala hakupinga, alisema kuwa anakuja na mimi nikamngoja kwa hamu ili nimuone atakavyokuwa.


Nikachukua ile pochi ya Lucy na kumkabidhi Suzy aiangalie kama alivyohitaji.
Suzy alishika ile pochi na kulala usingizi wa ajabu huku ile pochi ikiwa mkononi, alilala na kukoroma kabisa hadi mimi na Sam tukawa tunamcheka jinsi alivyokuwa akikoroma.
Mara mlango ukagongwa, nami nikaenda kufungua. Aliingia Lucy akiwa na nguo zile zile nilizomuona nazo awali, nikawa namuangalia kwa makini ambapo aliingia moja kwa moja ndani.
"Pochi yenyewe iko wapi?.


Nilishindwa kumjibu kwani nilikuwa nikimshangaa bado, Sam akamuonyesha kuwa ipo mikononi kwa Suzy, hapo Lucy akainama na kuibeba ile pochi.
"Mimi hata sio mkaaji jamani, tutaonana siku nyingine"
Akatoka na kuondoka, ni hapo Suzy nae akaamka.


"Mmh! Usingizi wa ajabu huu sijui hata umetokea wapi jamani. Hebu tuondoke Sabrina"
Kwakweli bado nilikuwa nachanganywa na vitu kichwani jamani kuhusu Lucy.
Suzy akainuka na kunikazania kuwa tuondoke, ikabidi tumuage Sam ambaye aliamua kutusindikiza.


Kufika kituoni, tukaona gari ikisimama na akashuka Carlos kisha akatufata na kuomba kutupa lifti.
Sam akakubali kwani alimuona Carlos kuwa mtu mwema, kisha mimi na Suzy tukapanda ile gari.
Nikamuomba huyo Carlos anipeleke mimi kwanza kisha Suzy afatie.
Suzy nae akahamaki kwa mshangao.


"Kheee! Kwanini asitangulie kunipeleka mimi halafu wewe ufatie?"
"Mi naona itakuwa vyema akianzia kwetu."
Carlos akacheka kwa yale mabishano yetu.
"Mbona mnaniogopa jamani? Mimi sio chinja chinja bhana, muwe huru tu.


Nikajifikiria na kuendelea kusisitiza kuwa nipelekwe mimi kwanza, mwisho wa siku akakubali.

Ile kufika kwetu gari ikasimama, wakati nashuka tu Suzy nae akashuka akidai kuwa hawezi kuongozana na mtu asiyemfahamu halafu peke yake ila Carlos aliendelea kusisitiza kuwa ampeleke tu.
Mara dada yangu Penina alikuwa anatoka ndani na kutukuta pale nje tukibishana, akauliza na tukamwambia tunachobishaniana. Dada Penina akamuangalia Suzy na kumwambia,
"Suzy, hebu panda twende wote hata mi nimefurahi kujipatia lifti hapa nje.


Ikabidi Suzy arudi tena ndani ya gari na dada na kuondoka.

Nikiwa ndani tumekaa na mama baada ya kula chakula na kufanya mambo mengine, mama akaanza kunilalamikia kuhusu dada.
"Siku hizi Penina amebadilika sana sijui hata ana matatizo gani na yeye."
"Kwani naye anawehuka kama mimi?


"Hapana ila ananiletea marafiki wa ajabu sana, leo alikuja na rafiki yake mmoja hivi yani ile kumuona tu hadi nywele zimenisisimka. Nikamuuliza Penina kama yule ni mtu wa kawaida kweli, akadai ndiye aliyempa zawadi ya mdoli eti hakuamini kama mdoli alichomwa ndio alikuja kuhakikisha"
Dada Penina nae akawa amerudi na alifikia moja kwa moja kwenye maongezi yetu.


"Unajua mama hata mi mwenyewe nimepatwa na mashaka na yule kijana, macho yake yapo juu juu halafu sina hata mawasiliano nae"
"Ulimkutia wapi sasa hadi kuja nae hapa nyumbani?"
"Nilimkuta stendi ndiyo kumueleza na kuja nae hapa, mmh unavyosema sio wa kawaida hadi unanitisha mama.
"Mnajiokotea tu marafiki wanangu, huenda akawa ni jini? Loh! Kutuletea majini hapa nyumbani wa nini?


"Mmeshaanza na stori zenu za majini tena! Mngejua ambavyo sizipendi hata msingeendelea."
Mama na dada wakacheka na kunitania kuwa mimi ni muoga tu.

Wakati wa kulala sikuweza kuendelea kukaa pale sebleni kwani mambo mengi yalitawala kichwa changu, nikaenda chumbani kwangu na kuona kama chumba changu kimekuwa kikubwa sana halafu mara nyingine nilihisi kama vile kuna uwepo wa mtu chumbani mule. Hofu ilikuwa imenijaa moyoni nikaamua kumpigia Sam simu ambapo niliongea nae na kujilidhisha kuwa yu salama huku nikitafuta usingizi bila kujenga mawazo kichwani mwangu, kisha nikalala.


Nikaona nipo kwa Sam, nikiwa na Suzy pale nje kama tulivyokuwa mchana na kumuona mtu akitoka chumbani kwa Sam ila hakuwa Lucy kama ambavyo nilimuona mchana bali alikuwa yule kijana wa ndotoni.
Halafu wakati nimempigia Lucy kuwa aje achukue pochi yake, aliyekuja hakuwa Lucy bali ni yuleyule mkaka.


Kumbe na ile pochi haikuwa pochi kama tulivyokuwa tukiiona bali lilikuwa ni jiwe linalowaka sana ndiomana Suzy alipoichukua ila aiangalia akashikwa na usingizi wa ajabu. Yote hayo nilikuwa nayaona wakati nimelala.
Nikawa mahali pengine, hapo nilikuwa nimekaa chini akatokea yule mkaka wa ndotoni na kusema.
"Asante Sabrina, leo nimefika kwenu.


Nikashtuka gafla kutoka ndotoni, hofu ikazidi kunijaa na uoga kunitawala nikaanza kujiuliza kuwa je huyo mkaka ndio yule ambaye mama alisema kuwa alikuja nyumbani na dada Penina au ni Carlos.
Bado nilikuwa na maswali mengi kichwani, mara nikasikia mtu akicheka mule chumbani kwangu hapo ndipo uoga hunitawala yani kati ya mambo yote usiombee kifanyike kitu ambacho hukioni kwa macho ya kawaida eti unasikia sauti tu ila ubaya zaidi ni kumuona afanyaye kama si binadamu wa kawaida unaweza ukazirai.


Kile kicheko kiliniogopesha sana, mara gafla kikatulia nikaamua kuchukua simu na kumpigia Sam ambapo niliongea nae hadi kunakucha ili kujiridhisha na uoga wangu.

Kesho yake jambo la kwanza likawa ni kumpigia Lucy simu ili niweze kujibiwa maswali yangu.
Ila simu haikupokelewa, nikaendelea na kazi zangu na badae Lucy akanipigia nami nikaanza kumuuliza alichokuwa anafanya kwa Sam jana ni kitu gani, Lucy akashangaa sana na kukataa kuwa jana hakuja kwa Sam.


"Acha uongo Lucy, nimekuona kwa macho yangu."
"Si kweli Sabrina, mara ya mwisho kuja kwa Sam ni siku ile uliyonifukuza. Tangia hapo sijafika tena kwa huyo Sam wako."
"Na ile pochi uliyoisahau siku ile si ndio uliifata jana Lucy?"
"Hapana, mi sijafika huko jana. Hata hivyo siku ile sikusahau kitu chochote huko sasa ningekuja kufata nini? Na pia nisamehe kwa siku ile, nilighafirika tu shoga yangu.


Nilikata simu na kuanza kujiuliza maswali kuwa inamaana ndoto niliyoota usiku ni ya kweli, vipi sasa ile ndoto niliyoota kwa Sam? Mbona alikuja Lucy siku hiyo na amekubali kuwa alikuja ila ya jana anakataa inamaana yule mkaka alijigeuza na kuwa Lucy? Hapo hofu ikanitawala na hata sikujua cha kufanya kwa muda huo. Nikatamani kumueleza mama ila maelezo yakawa yanagoma hata sikujua ni kwanini.

Jioni yake nilipigiwa simu na Suzy, akaanza kunieleza kuhusu Carlos.


"Yule mkaka alitaka namba zako jana ila nimemnyima"
"Vizuri sana, najua Sam nae hawezi kumpa namba zangu. Vipi dada Penina jana mlimuacha wapi?"
"Alishukia njiani, ila mimi nina mashaka na yule Carlos"
"Mashaka gani hayo?"
"Ngoja nimchunguze kwanza, nikipata jibu nitakwambia"
Mara nikamsikia dada yangu kama akipiga kelele hivi za kuniita, nikaacha kuongea na simu na kumkimbilia ili kujua kuwa nini tatizo.
"Mambo ya ajabu mdogo wangu."
"Yapi hayo?"
"Angalia mwenyewe"
Ilikuwa ni kwenye kompyuta yake kuna picha kama ile niliyomtolea mwanzo, akaniomba nimtolee tena.
Nikawa najaribu kuitoa, mara ikawa na sura ya yule mkaka wa ndotoni nikajikuta nikiacha na kukimbilia sebleni.


Nikawa kama vile sijielewi kwa kile kinachotokea, nikasikia simu yangu inaita nikaenda kuichukua, kuangalia namba mpya nikaipokea.
"Mambo vipi Sabrina?"
"Nani mwenzangu?"
"Carlos anaongea hapa.


Nikapatwa na mshtuko kuwa ameitoa wapi namba yangu. Nikiwa nawaza hilo, mara macho yangu yakatizama ukutani nikaona imebandikwa picha ya yule mkaka wa ndotoni.

Itaendelea kesho.......!!!!
Maoni yako ni muhimu sana mdau.
Kama tuko pamoja   
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:

 
 
Blogger Templates