NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 10:
Nikapatwa na mshtuko kuwa ameitoa wapi namba yangu. Nikiwa nawaza hilo, mara macho yangu yakatizama ukutani nikaona imebandikwa picha ya yule mkaka wa ndotoni.
Uoga ukatawala moyo wangu na kuanza kutetemeka, sikuweza tena kuendelea kuongea na ile simu.
Hofu ilizidi pale nilipoona kuwa ile picha ina tabasamu, uoga ulijaa zaidi nikaanza kupiga kelele na kuangusha simu yangu maana nilikuwa nimesimama basi ikaanguka hadi chini.
Mama aliyekuwa jikoni akakimbilia chumbani kwangu kujua kuna nini,
"Picha mama"
"Picha imefanyaje?
Nikamuonyesha pale nilipoiona ile picha ila haikuwepo tena.
"Inamaana uchizi wako umekurudia?"
Dada nae akaja chumbani,
"Mbona makelele Sabrina?"
Nikawa kimya, mama akanishika mkono na kunivutia sebleni ili kunipa moyo na kunipunguza uoga.
"Kwani unaizungumzia picha gani Sabrina?"
Dada nae akadakia.
"Tena Sabrina asante kwa kunitolea ile picha maana ilikuwa inanikera kweli yani"
Nikawa nashangaa kuwa nimeitoaje wakati ilinishinda kuitoa.
"Inamaana ile picha imetoka? Ila mi sijaitoa kwakweli"
"Sasa nani ameitoa?
Bado nilikuwa natetemeka kwa uoga, nikakumbuka kuwa simu yangu ilianguka.
Nikamuomba dada anisindikize chumbani kwangu nikaichukue ile simu, nikakuta kila kitu kipo kivyake.
Nikaiokoto na kuviunganisha, kujaribu kuwasha ikawa haiwaki dada akaniambia.
"Ishaharibika hiyo teyari, hakuna mawasiliano tena pole sana"
Roho iliniuma kweli kwa kuharibikiwa na ile simu ambayo nilikuwa naipenda.
Tukawa tumekaa sebleni, nikamuomba mama kuwa nitalala nae siku hiyo na muda wa kulala ulipofika nilienda kulala kwa mama.
Wakati tumelala nikamsikia mtu akiniita kwa sauti ya chini chini.
"Sabrina, Sabrina"
Nikashtuka usingizini, nikasikia tena akiniita, hapo uoga ukanishika. Nikamsogelea mama na kumkumbatia, nikahisi mtu akinishika mgongoni huku akiendelea kuniita, uoga ulinitawala kwani nilishindwa hata kujigeuza, nilikazana kumkumbatia mama kwa nguvu na sikumuachia kabisa, ndipo mama nae akashtuka.
"Kwani kuna nini Sabrina?"
Huku nikitetemeka kujibu,
"Kuna mtu mama"
Mama akainuka na kwenda kuwasha taa.
"Angalia sasa, yuko wapi huyo mtu? Hukupona wewe."
"Mama, alikuwa ananiita kabisa.
"Akuite nani usiku huu mwanangu? Mchawi? Maana wachawi ndio wanamchezo wa kuita watu usiku."
"Labda ni wachawi kweli mama, maana nilikuwa nahisi kuguswa mgongoni."
"Labda mzimu wa babako umekuja kututembelea leo"
Kauli ya mama ikanipa uoga zaidi, hata sijui kwanini yeye hakuogopa kuongea kauli kama zile usiku.
Akataka kwenda kuzima taa tena, nikamshikilia kuwa asizime taa.
"Unaogopa nini Sabrina? Mbona mimi siogopi kitu?
"Wewe mkubwa mama"
Akacheka, na kurudi kulala ila sikuweza kulala hadi panakucha.
Nilikuwa naona bora mchana kuliko usiku.
Kulipokucha kama kawaida dada aliondoka mapema sana kwenda kazini, mimi na mama tukabaki nyumbani.
Nikamvizia mama alipokuwa jikoni, nikaenda kuchukua simu yake ili kumjulisha Sam kuwa simu yangu imepata matatizo.
"Sasa itakuwaje Sabrina?"
"Ngoja nipeleke kwa fundi ila sina hela sasa sijui itakuwaje!"
"Ipeleke tu halafu utaniambia gharama za matengenezo nami nitakuletea hiyo pesa Sabrina, usipende kulalamika kitu ambacho mimi nina uwezo nacho"
"Sawa nimekuelewa.
Mama akaanza kuniita kwa nguvu.
Nikaweka simu yake na kumfata jikoni.
"Muda wote nakuita hauitiki au ndio ulikuwa unazungumza na mzimu wa babako"
Ikawa mara ya pili kumsikia mama kuhusu mzimu wa baba ikabidi nimuulize vizuri kuwa ana maana gani.
"Kwani mizimu huijui mwanangu?"
"Mi sijui mizimu mama"
"Mizimu ni viumbe ambavyo vipo tokea enzi za mababu na mababu, ni vigumu sana kumtendea jambo baya mtu mwenye mizimu kwani mara nyingi sana mizimu ile humuepusha nalo au humwambia kabla hajatendewa.
"Sasa mbona unasema mzimu wa baba? Inamaana baba kawa mzimu?"
"Mtu anapokufa huwa hawezi kurudi tena duniani ila kinachoweza kuzunguka na mzimu wa mtu huyo ambao huvaa sura ya muhusika."
"Inamaana kama huo mzimu wa baba utakuwa na tabia za baba?"
"Mzimu ule ulikuwepo na baba yenu enzi za uhai wake, kwahiyo unaporudi kwenu unakuwa kama yeye kwa kuwalinda watoto wake.
"Mmh mama hata sikuelewi, mizimu haitishi kweli?"
"Mizimu inatisha kweli mwanangu. Ipo hivi, kama mtu akimuua mtu asiye na mizimu basi haitampa shida sana ila akiua mtu mwenye mizimu atajuta maisha yake yote kwani itamtokea mara kwa mara na kumtesa.
"Kheee mama!! Na utajuaje kama huyu mtu ana mizimu au la? Mi naogopa sana"
"Usiogope mwanangu, kwenu kuna mizimu sana ipo siku nitakueleza vizuri zaidi. Baba yenu wakati wa uhai wake alikuwa akioteshwa na kuona mambo mengi sana yatakayotokea au kama yaliyotokea yametokea kwa sababu ipi. Ipo siku nitakwambia vizuri tufanye kazi kwanza."
Habari hii ya mizimu iliniingia sana akilini na kujikuta nikitamani kujua zaidi na zaidi, kama mizimu inatisha mbona mama anaitaja bila hofu na hata haogopi chochote? Nilitamani kujua mengi zaidi kuhusu hili jambo.
Baada ya kazi zote, alirudi dada Penina na leo tena aliwahi kurudi na kuanza malalamiko yake ya majini.
"Yani leo mama ndio live bila chenga tumekula chakula na majini"
"Ulikuwa na nani, halafu mmejuaje?"
"Nilikuwa na Fatuma mama, yani tumeagiza chakula kingi hilo ila hata hatujashiba. Fatuma akasema hatujasali ndomana hatujashiba, eti bila kusali majini yanakuja na kufakamia chakula."
"Na nyie mmezidi uroho, ila hizo ni imani tu. Ndio mkumbuke kusali kabla ya kula, maneno kidogo tu yatakusaidieni na kuwaepusha na vitu vibaya.
"Ndio, Fatuma kaniambia kuwa nikiona shida kufanya sala ndefu basi niseme Bismillah tu inatosha"
Mama akacheka sana,
"Wavivu utawajua tu"
Dada akainuka na kwenda kubadili nguo na mimi nikaendelea kutafakari kuwa kuna mambo mengi hapa, kwanza mizimu na pili majini kwakweli hali sio nzuri.
Usiku kama kawaida ilikuwa ni mtihani kwangu, leo mama akaniambia nilale mwenyewe na nisiwe na uoga wowote kwali ameshaniombea tayari. Nikamuomba dada tuangalie picha ya ngumi kwanza, ilivyoisha nikaingia chumbani kwangu na kulala kwani sikuwa na simu tena ya kuweza kuwasiliana na Sam.
Niliacha taa inawaka na kujifunika shuka gubigubi, usingizi haukukawia kunichukua.
Nilikuwa mahali kwenye nyasi nyingi nimekaa, huku nikisikia sauti ya mtu akizungumza na mimi.
"Sabrina, Sabrina. Wewe ni binti wa kipekee sana, unatakiwa uishi maisha ya kimalkia mwanadamu wa kawaida hawezi kufanya wewe uishi kama unavyotakiwa kuishi,
Nikashtuka toka usingizini, sauti nyingine ikaniambia kuwa nichungulie dirishani.
Nikasikia sauti ya paka nje, nikajua sauti inayoniambia nichungulie inataka nimfukuze yule paka.
Nikainuka na kufunua pazia la kwenye dirisha kwa uoga, nikamuona yule mkaka wa ndotoni amesimama karibu na dirisha halafu macho yake yanawaka kama taa.
Nikafunika lile pazia kwa uoga, nilihisi kutetemeka. Sauti nyingine ikasikika,
"Unaogopa nini Sabrina? Huyo ndio mumeo.
Nilizidi kutetemeka kwa uoga, nilitamani hata nibadilishiwe mazingira.
Wakati natetemeka, upepo ukaanza kuvuma chumbani kwangu kama vile niko nje, nilikuwa nimejikunyata kabisa mara nikasikia sauti ya paka tena,
"Nyau.... Nyaaau.... Nyaaau.... Nyaaau"
Kama vile yule paka ameingia ndani, nikazidi kutetemeka kwa uoga na gafla taa ikazimwa, halafu sauti ya yule paka akilia ikatawala chumba changu chote kwa hapo sikujua kilichoendelea tena jamani kwani nilizimia.
Niliona tu kumekucha na mama akiwa chumbani kwangu.
"Leo tena yamekupata yanayokupataga mwanangu?"
"Mama leo ndio makubwa zaidi, nilizimiwa hadi taa"
Mama akacheka sana kama kawaida yake,
"Nani akuzimie taa mwanangu? Uoga wako tu, umeme ulikatika leo"
Kwakweli chumba changu niliona kichungu wala maneno ya mama sikuyaelewa.
Mchana nikatoka nyumbani na kumpelekea fundi simu ile simu yangu kwani jana yake sikupata muda.
Niliporudi nyumbani nikabambana na maswali ya mama kuwa nimetoka wapi, nikamwambia kuwa nimetoka kwa fundi simu.
"Amekwambia sh. Ngapi?"
"Amesema ni elfu ishirini, simu ile imevunjika kioo cha ndani na nini sijui gharama yake ndio elfu ishirini.
"Unayo hiyo hela au unamtegemea yule pangu pakavu tia mchuzi wako akupe?"
"Mmh! Ndio nani huyo mama?"
"Si huyo Sam wako ambaye akijikuna anatoka unga, labda akakope. Na mimi ndio usifikirie kabisa kama nitakupa hiyo pesa"
"Mmh! Mama nawe unamdharau sana Sam"
"Nisimdharau ananisaidia nini hapa zaidi ya kero na karaha tu"
Nikaona kuzidi kuongea na mama kuhusu Sam ni kujiumiza mwenyewe ikabidi niwe kimya tu.
Badae nikamvizia mama na kuchukua simu yake kumpigia Sam kwani fundi alitaka na pesa ya kianzio kwanza ambayo sikuwa nayo kwa wakati.
Nikaongea na Sam na kumueleza kuhusu zile gharama,
"Sijui kama unaweza kuniamini Sabrina"
"Kukuamini kitu gani?"
"Bosi alinipa pesa za ofisi nikarudi nazo hapa nyumbani ili nipeleke benki, nimeenda kuoga ile kurudi sijakuta sh. Kumi yani kwa kifupi nimeibiwa wakati mlango niliufunga hata sijui cha kufanya, nimechanganyikiwa hapa. Halafu.......
Mama akanikuta nikiongea na simu yake akanipokonya na kuikata.
"Simu yangu ni muhimu kuongea na watu muhimu sio hao wachuja nafaka kama huyo Sam wako"
Nikatamani mama anipe simu ili nimuulize vizuri Sam kitu ambacho kimemsibu, ila sikuweza kwavile sikuwa na simu tena na wazo la kuikomboa simu yangu kwa fundi likapotea.
Nilikuwa ndani nimetulia, mama akaniambia kuwa nje kuna mgeni wangu amekuja kuniulizia.
Nikatoka nje kwenda kumuangalia ni nani.
Nikamkuta ni Carlos akiwa amesimama, nikasalimiana nae na maswali mawili matatu kisha akasema kuwa ameniletea zawadi, akafungua gari lake na kunitolea.
Kuangalia zawadi yenyewe ni simu, ikabidi nimuulize kuwa mbona kaniletea simu.
"Kwavile simu yako ilianguka na kuharibika nimeona ni vyema kukuletea nyingine."
Nilishtuka na kujiuliza amejuaje kama simu yangu ilianguka? Wakati hata Sam sikumwambia kama imeanguka zaidi ya kusema imeharibika tu?
Wasiwasi ukanijaa juu ya Carlos, nikataka nikimbilie ndani kwa mama.
Nilipogeuka ili kuondoka tu akanishika mkono na mkono wake ulikuwa wa baridi sana.
Itaendelea kesho.....!!!
Maoni yenu ni muhimu sana kwangu wadau.
Kama tuko pamoja
![]()
By, Atuganile Mwakalile

No comments:
Post a Comment