NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 11:
Nilipogeuka ili kuondoka tu akanishika mkono na mkono wake ulikuwa wa baridi sana.
Ubaridi ule ulipenya kwenye mwili wangu hata nilihisi baridi na mimi, Carlos akaniangalia kwa makini kana kwamba anayasoma mawazo yangu.
"Mbona unaniogopa Sabrina? Mimi ni binadamu wa kawaida kama wengine jamani."
Nilibaki nikimuangalia tu, bila ya kumjibu kitu chochote.
"Kwani mimi nina pembe jamani? Au natisha? Kwanini uniogope Sabrina?"
Nikazidi kumuangalia na kuanza kumuuliza maswali na mimi.
"Kwani wewe ulijuaje kama simu yangu ilianguka?"
"Kwahiyo hicho ndio kinafanya uniogope?"
"Na je namba yangu uliitoa wapi?"
"Sikia Sabrina, siku niliyochukua simu ya Sam kuweka namba yangu ndio nikachukua namba yako humo. Halafu siku ile niliyokupigia nilijua tu umeshtushwa na simu yangu kwani nikasikia kama simu imeanguka na gafla ukapotea hewani ndipo nilipogundua kuwa simu yako imeanguka na kuharibika.
Roho ikaniuma sana kwani mimi ndiye niliyesababisha ndiomana nikaamua kwenda kukununulia simu nyingine kama ishara ya kuomba samahani. Tafadhari Sabrina pokea simu hii"
Ingawa nimeyaelewa maelezo ambayo Carlos ameyatoa ila bado iliniwia vigumu kupokea ile simu.
Mara mama akatoka ndani na kunikuta nimesimama na Carlos pale nje.
"Yani Sabrina muda wote umesimama na mgeni hapo nje? Kwanini usiingie nae ndani mwanangu! Haya karibu ndani baba.
Nikajua mama ameshapagawa na lile gari la Carlos pale nje, ikabidi nimkaribishe Carlos ndani ingawa sikuwa na imani nae.
Tukiwa tumekaa pale sebleni, mama akaanza kumuuliza maswali mawili matatu Carlos.
"Kwani wewe ni mwenyeji wa wapi baba?"
"Mimi ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma"
"Wazazi wako wako wapi?"
"Wazazi wapo Kigoma ila nina ndugu zangu baadhi hapa na wazazi nao watakuja tu maana wamekaa sana kule na wameshapachoka"
Carlos aliongea mambo mengi sana na mama, hadi kumwambia kuhusu simu aliyoniletea.
Mama nae akaanza kunilazimisha kuwa nichukue simu ile niliyoletewa na Carlos.
"Yani mama, mi sina nia mbaya kabisa kumletea Sabrina simu. Nimefanya hivi kama ishara ya urafiki wetu tu.
"Ndio namshangaa hapa kinachomfanya akatae, labda anahisi utamdai."
"Siwezi kumdai mama, nimemletea hii simu kwa hiyari yangu mwenyewe"
Mama akaendelea kunisisitiza kuwa niichukue, ikabidi niichukue ile simu na kumuuliza swali ambalo lilinitatiza bado.
"Mbona mikono yako ni ya baridi sana?"
"Hutokea tu ila si mara zote, nadhani nina upungufu wa madini flani mwilini"
Mama akaanza kucheka kisha Carlos akaaga na kuondoka.
Nilitafakari vitu vingi sana bila ya kupata jibu, kwakweli huyu Carlos alinifikirisha sana tena sana, hata nikashangaa kuwa mama amewezaje kumuamini Carlos kwa muda mfupi kiasi kile.
Mama akaja na kuanza kuniambia.
"Maskini jeuri wewe, simu unaitaka halafu unavunga! Kaka wa watu kajitokea mbali kwaajili yako eti wewe unavunga loh"
"Ila mimi simuamini yule kaka kabisa"
"Kwanini humuamini? Mbona ni mtu wa kawaida tu mwanangu!"
"Mi simuamini tu jamani"
Kwakweli sikumuamini kabisa Carlos niliona ni majanga tu.
Usiku ulipofika, mama alikuja kutembelewa na rafiki yake mama Salome.
Mama akaanza kumuelezea kuhusiana na matatizo yangu ya kuogopa ndani.
Nilikuwa kimya kwenye kochi nikijifanya nimesinzia ila nilisikia yote waliyozungumza.
"Sasa mama Penina, kama mtoto anawehuka hivyo wakati wa kulala kwanini msifanye maombi?"
"Hapo ndio hadi mi mwenyewe najishangaa mama Salome, yani Sabrina akianza kuwehuka huwa sikumbuki kabisa kusali hata sijui kwanini?
"Dunia imechafuka sana ndugu yangu, shetani ana jeshi lake kubwa humu duniani inatakiwa mkumbuke kusali kwani sala ni nguzo imara ya kumpinga shetani."
"Asante mama Salome nitafanyia kazi ulichosema"
"Tena kwa ushauri wa bure, ita familia yako tulia nayo mnaomba pamoja halafu mnalala"
"Nimekuelewa ndugu yangu.
Mama Salome akaaga na kuondoka kwani alikuja kumwambia mama habari za kikundi chao ila mazungumzo haya mengine yaliingilia kati tu.
Dada akarudi nyumbani, kwakweli leo alichelewa sana kurudi na alitukuta tunakula ilibidi mama amuulize sababu ya kuchelewa.
"Kuna mambo ya Fatuma namsaidia kushughulikia, nadhani kesho au keshokutwa tunaweza kufanikisha"
"Mambo gani hayo?"
"Nikiyasema sasa hivi kuna shoga yangu hapa atasema namtisha asilale, nitawaambia kesho kama nikirudi mchana"
Nikajua tu hayo mambo lazima yatakuwa yanahusiana na majini tu ndiomana hajayaongelea kwani anajua kuwa mimi naogopa sana mambo hayo.
Muda wa kulala ukafika, mama akainuka kwenda kulala na kuniacha na dada pale sebleni. Nikakumbuka maneno ya mama Salome kuwa tupende kusali kabla ya kulala, nikamfata mama na kumwambia kuwa amesahau maagizo aliyosema kwa mama Salome kuwa atayatelekeza.
Nikamkumbusha mama kusali naye akakumbuka, akarudi sebleni na kumwambia dada Penina kuwa tunatakiwa kusali kabla ya kulala.
"Mama, kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe, maswala ya kulazimishana kusali mimi hata siyapendi"
Dada Penina akawa anapinga kabisa ikabidi mama amuombe na kumlazimisha kuwa ni vyema tukifanya ibada ya pamoja, badae akakubali.
Kama familia tukaamua kufanya ibada kabla ya kulala.
Wakati wa ibada hiyo hakuna aliyeelewa nini kiliendelea kwani kila mmoja alijikuta yupo chumbani kwake asubuhi, na mama ndiye aliyekuwa wa kwanza kuja chumbani kwangu.
"Hivi muda ule tuliosema tunafanya ibada ilikuwaje?"
"Hata sielewi mama, maana sina kumbukumbu za ibada hiyo."
"Mmh ya leo kali!"
Dada Penina nae aliamka na kuja chumbani kwangu.
"Leo nimechelewa hadi kwenda kazini sijui hata ni usingizi wa aina gani!"
"Kila mmoja anashangaa hapa maana mara ya mwisho tulipanga kufanya ibada"
"Au tulifanya ibada na kwenda kulala?"
"Labda ila hakuna mwenye kumbukumbu yoyote."
Mimi nilikuwa natafakari tu na nikatambua kuwa yote yanafanywa na yule mkaka wa ndotoni tu kwani tuo afanyaye mambo ya ajabu.
Mchana nikampigia simu Sam, ambaye alikuwa na mawazo ya kupotelewa na pesa ya ofisi.
"Yani nimechanganyikiwa Sabrina, hata sijui pesa ya ofini nitaipatia wapi tena jamani mmh!"
Nikajaribu kumpa moyo na kumwambia maneno mazuri ambayo najua hayakumfariji hata kidogo kwani alikuwa ameshachanganyikiwa.
Nikapigiwa simu na rafiki yangu Suzy ambaye alianza tena kuniuliza kuhusu Carlos.
"Sabrina, unamuonaje Carlos?"
"Namuona ni mtu wa kawaida tu, kwani wewe unamuonaje?"
"Ngoja kwanza, nikimaliza uchunguzi wangu nitakwambia"
Suzy akakata simu, nikajiuliza maswali kuwa kwanini Suzy ana wasiwasi juu ya Carlos.
Mama akaniita na kuniambia kuwa ameongea na kaka na amesema kwamba hivi karibuni atanihitaji kwake ili nikabadilishe mazingira kidogo, kwakweli nilifurahi sana, hata dada aliporudi aliona jinsi nilivyofurahi.
Wakati wa kula dada akaamua kunitani,
"Naona umefurahi kuepukana na stori zangu za kutisha."
Mama akadakia,
"Lazima afurahi, anavyoogopa majini na watu waliofufuka huyu balaa"
Yani wanavyosema watu waliofufuka mie mwenzao ndio nazidi kupatwa na uoga wa mawazo.
"Anaogomba mazombie mdogo wangu jamani, ila mama yanatisha kweli yale usiombe ukutane nao
"Majini yako je hayatishi?"
"Mama wee usiniambie habari za majini, kilichompata Fatuma ni balaa"
"Mmeshaanza stori zenu sasa, mi mnanikera sana"
Ikabidi wanyamaze na tuendelee kula kama kawaida.
Usiku mawazo yangu yalikuwa ni kwenda kwa kaka tu, sikuwa na mawazo mengine zaidi ya hayo na sikutaka kukaribisha mawazo ya zaidi.
Wakati wa kulala ulipofika, nilikwenda chumbani na kulala moja kwa moja hata simu sikuongea nayo usiku.
Nikamuona Sam akihangaika sana, mara nikamuona akifunga ndoa na Lucy halafu tena nikamuona akitokwa na majipu mwili mzima. Nikashtuka kutoka kwenye ile ndoto na kujikuta nikianza kuogopa mule nyumbani, kwani wakati nimeshtuka nilikuwa nahisi kama mtu akitembea tembea mara avute kiti mara avute meza halafu sauti ikasika.
"Mbona umeamka kabla ya wakati Sabrina?"
Uoga ukanijaa, nikakumbuka maneno ya mama Salome kuwa natakiwa kusali.
Nikashuka kitandani na kupiga magoti, kabla sijafanya chochote taa ya chumbani ikazimwa halafu mikono ya baridi ikawa inagusa miguu yangu.
Kwakweli nilitetemeka kiasi cha kupoteza fahamu, sikupenda kutazama mbele na mara taa zikawashwa tena hapo nilizidi kutetemeka na hakuna maombi tena niliyoweza kuyafanya.
Nilijikunyata ukutani bila ya kujua cha kufanya, ile sauti ikajirudia tena.
"Mbona umeamka mapema Sabrina"
Kwakweli huu usiku ningeweza kuubadilisha basi ningeubadilisha jamani, jasho jingi lilinitoka na wakati nilikuwa natetemeka kwa baridi la uoga.
"Usiogope Sabrina, nipo nje ya chumba chako bado sijaingia ndani ila karibia nitaingia"
Mara gafla nikaona mlango wa chumba changu ukifunguliwa, muda huohuo mkojo ulinitoka bila ya hodi.
Itaendelea kesho......!!!
Kama tuko pamoja
![]()
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:
Post a Comment