Social Icons

Tuesday, 20 June 2017

HADITHI; Niliolewa na Jini bila ya kutarajia - 12


NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 12

Mara gafla nikaona mlango wa chumba changu ukifunguliwa, muda huo huo mkojo ulinitoka bila ya hodi.
Nilikuwa nangoja kuona huyo mtu wa ajabu atakayeingia ndani kwani nilijua kuwa kwa vyovyote vile siwezi kumkwepa.


Mlango wangu ulikuwa unafunguliwa polepole, ujasiri ukaniisha na kujifunika sura kwani sikuweza tena kutazama kitu kitakachoingia, mara nikashikwa kichwani na hapo nikapiga ukelele uliomuamsha hadi mama.


Mama akafika chumbani kwangu wakati mimi nikiwa bado nimeinama na kujikunyata.
"Vipi mwanangu jamani? Umepatwa na nini tena? Eti Penina, mdogo wako amepatwa na nini?"
Mama alimuuliza dada Penina ambaye naye alikuwa chumbani kwangu.


"Hata mimi namshangaa jamani, mi nilikuja chumbani kwake huku na nikafungua mlango taratibu ili nisimsumbue, shida yangu ilikuwa ni ile pochi ndogo. Nimeshangaa kumkuta hapo chini amejikunyata na kujiinamia nikaamua kumshika kichwani ili kumuangalia ana tatizo gani ila ile kumshika tu ndio akapiga makelele yote hayo.


Mama akaniangalia kwa makini,
"Kwani una nini Sabrina? Au kuna mambo ulikuwa unayawaza?"
Kitu cha kwanza kuwauliza ilikuwa ni muda,
"Kwani saa ngapi saizi?"
"Kumekucha mwanangu na dada yako ndio huyu amejiandaa kwenda kazini"
Nikabaki nashangaa tu na sikuelewa chochote, mama akaangalia chini na kuona yale majimaji ya mkoje.


"Kheee! Hadi umejikojolea Sabrina!! Ulikuwa unaogopa nini mwanangu?"
"Amejikojolea kweli loh"
Dada akaanza kucheka, kisha akachukua alichosema na kuondoka.
Nikabaki na mama tu pale ndani.


Kulipokucha vizuri nilikuwa nimeshaoga na kutafakari ya usiku kwakweli hakuna ambacho nilikuwa nakielewa. Nikaenda kwa mama jikoni kumuuliza,
"Nitaenda lini kwa kaka Deo mama?


"Sabrina mwanangu, umeanza uoga hadi wa kufikia kujikojolea si utaenda kutia aibu tu huko kwa kaka yako? Sidhani kama wifi yako atavumilia hali hiyo!"
"Mama yani bahati mbaya ya siku moja ndio unaihesabia kama siku zote? Mimi nataka kwenda kwa kaka haijalishi nini wala nini"
"Utaenda ila ndio hivyo utatutia aibu kama ukiendeleza hiyo tabia"
Nikamsikiliza mama ila moyoni bado nilitaka kwenda kwa kaka tu ili nibahatike kubadilisha mazingira kidogo.


Mchana nikajilaza sebleni kwani macho yangu yalikuwa mazito sana na kujawa na usingizi.
Mama akanishtua kuwa nimepata ugeni, kuamka nikamkuta ni Carlos ambapo mama alimkaribisha sebleni tayari.


Kisha mama akaenda chumbani kuendelea na mambo yake mengine, Carlos akaanza kujiongelesha pale.
"Mbona umechukia Sabrina? Hujaupenda ujio wangu?"
"Hapana, ila mbona umekuja bila taarifa?"
"Nimekuja kuangalia unaendeleaje Sabrina, nakujali sana mama angu. Nikwambie kitu Sabr."
"Niambie tu hakuna tatizo"
"Sabrina, wewe kweli ni binti mzuri na mrembo yani ingawa umetoka kulala ila bado unapendeza na kuvutia. Sura yako ina mvuto wa hali ya juu Sabrina, na umbo lako ni zuri sana ila samahani kama sifa zangu zimevuka mipaka.


Nikacheka na kumuangalia vizuri huyu Carlos ambaye leo alikuja na staili ya kunisifia.
Nikaamua kumuuliza swali Carlos,
"Mbona umeamua kunisifu kiasi hicho?"
"Anayestahili sifa acha apewe sifa yangu, kwakweli Sabrina hadi nimekupenda yani."
Nikashtuka na kumuuliza tena.


"Si unajua kama mimi nipo na Sam halafu tunapendana sana?"
"Tatizo lenu wasichana ndio hilo, mtu akitamka nakupenda basi wewe ushapelekea kwenye maana nyingine. Mimi nakupenda Sabrina kama Sabrina na si vinginevyo.


Nikabaki kimya kwani alinishushua, akaongea mambo mengine kisha akaondoka.
Nikawa naitafakari ile kauli ya Carlos ya kusema kuwa ananipenda Sabrina kama Sabrina na si vinginevyo, kauli yake bado ilikuwa na utata sana kichwani mwangu ila sikupenda kuijadili zaidi.

Jioni yake Carlos akanipigia simu na kuniuliza.


"Unapenda chocolate Sabrina?"
"Ndio nazipenda."
"Nikuletee?"
Nikasita kuitikia nikawa kimya tu na simu sikioni,
"Basi nakuletea"
Halafu akakata simu, nikawa nashangaa tu kwani bado sikuwa na imani nzuri na Carlos.
Haikuchukua muda nikamsikia Carlos akizungumza na mama.


"Mimi sio mkaaji mama, nimemletea Sabrina mzigo wake huu."
Kisha nikamsikia akiaga, baada ya muda kidogo mama akaniita huku akiufungua ule mzigo.
"Mmh kumbe chocolate, huyu ndio mkwe bwana sio huyo Sam wako."
Akafungua moja wapo na kuanza kula huku akinikabidhi ule mfuko, ila mimi nikakataa na kumuachia mama.


Dada yangu Penina nae aliporudi wakaungana na mama kula zile chokleti. Na mimi nikatumia mwanya huo kumchombeza mama,
"Leo mama tutalala wote eeh!!"
"Hakuna shida mwanangu tutalala tu, ila masharti yale yale kuongea na simu usiku sitaki."
"Sawa mama hakuna tatizo"
Nikatulia pale sebleni na kuwaangalia tu walivyokuwa wakisakamia zile chokleti huku wakisifu kuwa ni tamu sana.


Usiku ulipowadia, nilijipanga kulala na mama ila nilimkumbuka sana Sam nikaamua kumpigia simu kabla ya kulala ila haikupatikana.
Mawasiliano yangu na Sam yamekuwa yakisuasua sana kwa siku mbili tatu hizi hata nikishindwa kuelewa kuwa Sam atakuwa amepatwa na tatizo gani jingine.


Nikaenda kulala chumbani kwa mama ambaye alinisihi kuwa nisiwe muoga, kitu cha ajabu kwetu ilikuwa tunakumbuka vyote ila si kusali tena mara nyingine kukishakucha mama ndio anakumbuka kuwa hakufanya ibada.


Niliongea na mama pale mambo mawili matatu na kisha kulala.

Kama kawaida yule mkaka wa ndotoni alinitokea na kunifata mahali ambapo nilikuwa nimekaa katikati ya nyasi laini na nyororo, yule mkaka akaanza kusema.
"Nikupe kitu gani Sabrina ili ujue kama nakupenda? Nikuonyeshe ishara gani ili utambue upendo wangu kwako?


Nikawa namuangalia tu bila ya kumjibu chochote kile.
"Ninauwezo mkubwa sana wa kukufanya mke wangu hata kama hutaka ila mimi nahitaji ukubali kwa hiyari yako mwenyewe"
Akaanza kuongea maneno ambayo yalifanana na aliyoongea Carlos mchana.
"Sabrina, wewe ni binti mzuri na mrembo. Una sura ya kuvutia na umbo."
Kisha akamalizia kuwa.


"Anayestahili sifa apewe sifa yake"
Nikashtuka kutoka usingizini na kuhema juu juu.
Nikaanza kumfikiria Carlos, sura yake ikatembea mawazoni mwangu na ule ubaridi wa mikono yake nikaanza kuuhisi mwilini mwangu hadi kuanza kutetemeka.


Nikajiuliza maswali mengi sana juu ya Carlos, mara nikaona kivuli cha mtu mule chumbani kwa mama hapo sasa uoga ukanishika na kuanza kutetemeka, kile kivuli kikawa kinanisogelea taratibu yani kinakuwa kirefu nikawa nimemkumbatia mama na mara ikasogea hdi usoni kwangu na kunichekea.


Hapo sasa nikaanza kumuamsha mama kinguu ila mama alikuwa hoi kabisa hata hajitambui na hakuamka kabisa ikawa kama vile niko peke yangu mule chumbani.
Ikaanza sauti ya paka kama ile ambayo uwa inasikika chumbani kwangu, hapo nikazidi kutetemeka na kuzidi kumkumbatia mama.


Kwakweli leo nilimshangaa mama kwani hakushtuka hata kidogo tofauti na siku zingine, na gafla umeme ukakatika hapo ndipo uoga ulipozidi na kuendelea kumuamsha mama ambaye aliamka na kuongea kama mlevi kisha kulala tena.


Katika hali ile ya uoga nikapitiwa na usingizi palepale.

Yule mkaka wa ndotoni alikuwa anacheka sasa tena akicheka sana sana, kisha akaniambia nimpe mkono wangu nikasita kumpa na kukataa kabisa, akaniambia.
"Nakupenda Sabrina"
Nikamuangalia tu, akawa analazimisha kuwa nimwambie nampenda nikagoma akawa anataka kunichukua kwa nguvu.


Nikashtuka na kupiga kelele,
"Nampenda Sam"
Hapo mama nae akashtuka na kuniangalia kwa jicho kali sana.
"Yani wewe asubuhi Sam, mchana, jioni khee hadi ndotoni? Huyo Sam kakupa nini mwanangu?"
Akiuliza hayo, alikuwa akiangalia mwanga uliokuwemo chumbani na kugundua kuwa kumeshakucha teyari, akastaajabu sana kuona amepitiliza kulala kiasi kile.


Nikaenda kumuangalia na dada Penina ambaye nae alikuwa hoi na usingizi, nikamuamsha naye alishangaa kuona kumekucha kuasi kile.
"Mmh nimelala kama mlevi leo jamani"
Nadhani na wao hawakujielewa kama mimi niotaye ndoto za ajabu tu.


Siku ya leo kila mtu alikuwa na mawazo nyumbani kwetu, sijui na wao walipatwa na mandoto ya ajabu kama yangu. Nikawa nimetulia na kutafakari, ikaingia simu kuangalia mpigaji ni Lucy. Ile kupokea tu akanipachika swali,
"Sam unampenda humpendi?"
"Swali gani hilo la kuniuliza Lucy?"
"Kila swali ni swali na linahitaji majibu, jibu swali nililokuuliza.


"Unajua wazi jinsi gani nampenda Sam"
"Kama unampenda mbona unamsababishia majanga?"
"Majanga? Majanga gani?"
Lucy akakata simu, nikajaribu kumpigia Sam hakupatikana.


Nikampigia tena Lucy naye hakupatikana na kujikuta nikiwaza vitu vingi mno.

Nikafikiria sana na kukosa jibu, nikaamua kuvaa ili niende kwa Sam.
Kwavile ilikuwa ni jioni sana yani karibia na usiku, mama akanikatalia kutoka. Nikajikuta nikiwa na mawazo sana na roho kuniuma, muda wote nilimjaribisha hewani Sam alikuwa hapatikani wala Lucy nae hapatikani.


Siku hiyo nilikaa na dada kwenye luninga huku nikiwa na mawazo tu, ila badae dada alienda kulala na kuniacha mwenyewe pale sebleni. Saa sita usiku nikaamua kumtafuta tena Sam hewani na muda huu simu yake ikaita nikafurahi sana ili niweze kuongea naye na kupunguza mawazo yangu ila cha kushangaza hakupokea Sam bali ilipokelewa na Lucy.


"Sema shida yako haraka tunataka kupumzika bhana."
Niliiweka ile simu sikioni huku nikiwaza kuwa huyu ni Lucy kweli au yule jamaa wa kujigeuza. Mara nikashikwa bega na ile mikono ya baridi.

Itaendelea kesho......!!!!
Kama tuko pamoja   
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:

 
 
Blogger Templates