Ukizichakata vizuri nadharia zilizomfanya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kukatwa mapema kwenye kinyang’anyiro cha urais CCM mwaka 2015 ni tabia ya kudhihirisha nguvu na silaha zake.
Lowassa alijiweka wazi kwa kila kitu kiasi kwamba iliwapa urahisi viongozi wa juu wa CCM waliokuwa na malengo ya kumzuia asipate tiketi, kujua ni wakati gani katika mchakato na hatua ipi ya kumuondoa.
Hata kwa mfuatiliaji wa juujuu alijua kabisa kuwa nguvu na jeuri ya Lowassa kuelekea kuipata tiketi ya CCM kuwania urais ilikuwa kwa viongozi wa CCM wa mikoa, wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (Nec), vilevile Mkutano Mkuu.
Lowassa akijionyesha wazi hivyo, alikuwa anafahamu wazi kwamba kikwazo chake kikubwa kuelekea kuwa Rais wa Tanzania kilikuwa tiketi ya kuwa mgombea urais wa CCM, kisha kikwazo cha kuipata tiketi hiyo ni uongozi wa juu wa chama.
Sasa basi, kanuni ni kwamba unapokuwa kwenye mapambano ya aina yoyote yenye alama za vikwazo hupaswi kudhihirisha nguvu zako. Endapo kikwazo kinakuwa ni watu wenye nguvu kuliko wewe, kuonyesha japo chembe ya uimara wako ni hatari sana.
Kuelekea kuitwaa tiketi hiyo, Lowassa alikuwa anakabiliwa na kikwazo cha watu ambao si tu walikuwa na nguvu ya kulazimisha uamuzi kwenye chama, bali pia walikuwa na mamlaka makubwa kwenye nchi.
Kati ya mbinu 36 za kushinda mapambano zilizochorwa karne ya tano na Jenerali wa China ya Kale upande wa Kusini (Southern Qi), Wang Jingze na kuwekwa kwenye kitabu cha Qi , ile ya kwanza ingemsaidia Lowassa.
Baada ya Mfalme Gao kufariki dunia, alifuata mjukuu wake, Mfalme Xiao Zhaoye ambaye alimteua mjomba wake, Xiao Luan kuwa Waziri Mkuu. Xiao Luan alimpindua Mfalme Xiao Zhaoye (mpwa wake) na kumuua kwa hoja kuwa alikuwa hatoshi ufalme.
Xiao Luan ndiye Mfalme Ming ambaye baada ya kujitangaza Mfalme wa Southern Qi, alianza kuua watu ambao walikuwa ni ndugu damu ya moja kwa moja kutoka kwa Mfalme Xiao Zhaoye mpaka Mfalme Gao. Alitaka kukifuta kizazi chote ili abaki salama.
Wang Jingze alipoona mnyororo wa vifo, alijua naye zamu yake ya kuuawa imewadia, ndipo alipozama chini kuandika mkakati wenye mbinu za kumpindua Mfalme Ming.
Mkakati huo ndiyo ambao nautumia hapa kuonyesha jinsi nadharia zake kama zingetumika, Lowassa angeweza kushida tiketi ya kuwa mgombea urais CCM 2015 kisha kuwa Rais.
Somo lililompita Lowassa
Katika mbinu hizo, ya kwanza inasema vuka bahari bila ufahamu wa mfalme. Hapo Wang alimaanisha kuwa kwa sababu alikuwa kwenye mapambano na mfalme, yaani mtawala, ilikuwa lazima apange mipango yake bila kumfanya Mfalme Ming amshutukie. Unaficha lengo kuu, ukitanguliza lengo bandia ili adui asikushtukie unataka nini.
Wang alikuwa Jenerali wa Southern Qi, hivyo vikosi vya jeshi la China Kusini vilikuwa chini yake, kutokana na uwezo huo, ingedhaniwa yeye kumpindua au kumuua Mfalme Ming ni rahisi. Hata hivyo, alitambua nguvu ya mfalme, ndiyo maana alituliza kichwa na kuandika mbinu hizo 36.
Lowassa alifahamu kuwa Rais Jakaya Kikwete hakuwa radhi naye kuelekea kuwa mgombea urais wa CCM na hatimaye kuwa Rais. Kikwete pia ndiye alikuwa mwenyekiti wa CCM.
Kwa kutambua hilo, Lowassa alipaswa kumheshimu na kumhofia zaidi Kikwete maana alikuwa na nguvu nyingi za kuzuia ndoto zake za kuwa Rais. Kwa maana hiyo, Lowassa alipaswa kufanya siasa za kumzunguka Kikwete, bila kumwonyesha mahali nguvu yake ilipo.
Lowassa alipaswa kuvuka bahari bila Kikwete kujua. Ilitakiwa Kikwete kila akisaka alama za uimara wa Lowassa azikose. Hiyo ingempa wakati mgumu wa kujua mahali pa kimdhibiti.
Mathalan, Lowassa alikatwa kabla ya kufika kwenye mkutano wa Kamati Kuu uliotakiwa kupitisha majina matano ya kwenda Nec ambayo ilichagua watatu kuingia Mkutano Mkuu.
Uamuzi wa kukata jina la Lowassa kabla ya kuingia Kamati Kuu, ulisababishwa na ukweli uliokuwa wazi kwamba nguvu yake ilikuwa kubwa kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu mpaka Mkutano Mkuu.
Kwa maana hiyo, Lowassa alivuka bahari kwa kelele, hivyo kumshtua mwenyekiti na vigogo wa chama ambao waliamua kumkabili kwa kumuondoa kwenye kinyang’anyiro kabla ya kuingia kwenye maeneo ambayo Lowassa aliyategemea sana.
Tafsiri kila hatua na ‘chachandu’ za kisiasa ambazo Lowassa alinogesha mwaka 2015, mpaka akaonekana tishio, Kikwete aliona siyo kitu kwa sababu alijua mahali pa kumdhibiti. Usipambane na mwenye mamlaka ukimwonyesha jeuri yako ilipo.
Sura ya tatu ya mbinu za kushambulia, ya pili ‘Borrow a corpse to resurrect a soul’. Tafsiri isiyo rasmi ni kodisha maiti ufufue nafsi. Hata hivyo, kile ambacho Wang alikimaanisha ni kuwa ukishajua mbinu za adui unazikodi kisha unazitumia au timu yake pia unaichukua.
Mtu hawezi kuifahamu timu unayoitegemea kama hujajiweka wazi. Ndiyo maana baada ya Lowassa kukatwa CCM, Kikwete aliwachukua watu wake muhimu kama Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na wengine kisha kuwapa majukumu muhimu dhidi yake.
Nchimbi na Sophia wote waliingizwa kwenye timu ya kampeni za ushindi wa Dk John Magufuli aliyepitishwa na Mkutano Mkuu kuwa mgombea urais. Huu ndiyo ufufuaji nafsi wa timu ya Lowassa uliokuwa umekatishwa tamaa na uamuzi wa chama.
Kikwete alifanya makusudi kuhakikisha Lowassa anapoondoka CCM, watu wake wenye nguvu kwenye chama wanabaki na kufanya kazi ya kupigania ushindi wa mgombea wao wa urais dhidi ya mtu ambaye walimtaka.
Ni hapo ikashuhudiwa Nchimbi anasimama jukwaani kumnadi Rais Magufuli dhidi ya aliyekuwa mtu wake. Akina Sophia wakawa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake CCM ili kukipa ushindi chama dhidi ya Lowassa, japo kwa shingo upande.
Kwa uamuzi huo, kile kishindo cha Lowassa kuhama CCM akiwa na msululu wa watu wazito kikadhibitiwa. Watu wake muhimu walifahamika na walidhibitiwa, kisha kutumika CCM dhidi yake.
Lowassa na Uhuru Kenyatta
Katika Uchaguzi Mkuu Kenya uliofanyika Agosti 8, mwaka huu, Lowassa alijipambanua wazi kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta ambaye ametetea kiti chake cha urais dhidi ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.
Lowassa hakuishia kumuunga mkono Uhuru kwa maneno, alisafiri mpaka Kenya na kuhamasisha jamii ya Wamasai kumchagua Uhuru, akitoa sababu kuwa Raila alimsaidia Rais Magufuli kushinda dhidi yake mwaka 2015.
Laiti Lowassa angejua athari za yeye kupanda jukwaani kumnadi Uhuru katika maisha yake ya kisiasa, asingefanya hayo. Pengine alichokifanya ni kumkomoa Raila au kumwonyesha Rais Magufuli kuwa anao marafiki wakubwa kisiasa. Amekosea.
Msisitizo kwake ni kuvuka bahari bila mfalme kujua. Rais Magufuli kwa sasa ndiye mkuu wa nchi. Ikiwa Lowassa ana nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2020, anaweza kujikuta analipa gharama kubwa kwa kitendo chake cha kupanda jukwaani Kenya kumfanyia kampeni Uhuru.
Bila shaka Lowassa anaweza kuhitaji msaada kutoka kwa Uhuru atakapokuwa anagombea urais. Hapo unapiga hesabu kuwa kutoka Agosti 2017 mpaka Oktoba 2020 ni zaidi ya miaka mitatu. Uhuru na Magufuli ni marais katika nchi jirani, zenye kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais Magufuli anaweza kwa kutumia nafasi yake kuhakikisha urafiki wa Uhuru na Lowassa unafutika. Magufuli anaweza kumuweka Uhuru karibu na kufanya naye mipango mikubwa. Uhuru anaondoka madarakani mwaka 2022, hivyo kwa mipango akawa anatamani zaidi Magufuli arejee madarakani ili waikamilishe pamoja.
Siyo kwa kutumia nguvu, ni ushawishi tu katika mbinu za medani. Lowassa atajikuta anaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu 2020, huku watu ambao aliwategemea hawapo naye.
Katika mbinu za kushambulia, ya sita inasema; ‘defeat the enemy by capturing their chief’. Yaani mshinde adui kwa kumteka chifu wao.
Mbinu hii humaanisha kuwa badala ya kumkabili adui moja kwa moja, unamtazama yule mkuu wake anayempa jeuri ya kifedha au mbinu, kisha unamteka. Magufuli anaweza kumteka Uhuru kwa mipango mikubwa na nafasi anayo. Ni Rais wa nchi.
Kati sura ya nne katika mbinu hizo, ya kwanza inasema; ‘remove the firewood from under the pot’. Yaani ondoa kuni chini ya chungu. Tafsiri; si unataka kutibua kilichomo kwenye chungu? Ondoa kuni chakula kisiive. Rais Magufuli akiona kuni inayompasha moto Lowassa ni Uhuru, ataiondoa tu chini ya chungu.
No comments:
Post a Comment