KRais Uhuru Kenyatta amewasilisha majina ya mawaziri aliowateua kwenye Bunge la Taifa kwa ajili ya kuidhinishwa kutumikia nyadhifa hizo.
Kupitia kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, Rais Uhuru Jumatatu amewasilisha majina ya mawaziri tisa, makatibu wakuu saba na mabalozi saba kwa ajili ya kuidhinishwa au kukataliwa kabla ya kuanza kutumikia nafasi hizo.
Walioteuliwa katika Baraza la Mawaziri ni Margaret Kobia - Vijana na Utumishi wa Umma, John Munyes - Madini na Mafuta, Monica Juma -Mambo ya Nje, Simon Chergui – Maji, ), Rashid Achesa – Michezo, Farida Karoney – Ardhi, Ukur Yattany – Kazi, Peter Munya - Jumuiya ya Afrika Mashariki, Keriako Tobiko – Mazingira.
Wakati huo huo Mwanaharakati wa Haki za kibinadamu Okiya Omtatah amefika mahakamani Jumatatu kupinga nafasi mpya za katibu mkuu wa utawala iliyobuniwa na Uhuru Kenyatta, akidai kuwa ni kinyume cha katiba.
Katika ombi lake alilopeleka kwenye mahakama za sheria za Milimani, Omtatah ametaja kukosekana kushirikishwa wananchi katika maamuzi ya kuingiza nafasi hizo mpya katika kuwasaidia mawaziri na majukumu yao.
Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo, “kuwekwa kwa nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa Utawala katika wizara zote za serikali kwa kushauriana na Kamisheni ya Utumishi wa Umma (PSC) ni batili.”
Ameitaka mahakama kubatilisha uamuzi wa rais na kuamrisha Muturi kutopokea au kuyajadili majina ya wateuliwa atapoletewa.
Ijumaa wakati Rais akitangaza orodha ya Baraza la Mawaziri, alieleza kuwa “Makatibu Wakuu wa Utawala atakuwa na jukumu pana la kuwasaidia mawaziri katika kuratibu kwa ubora zaidi uendeshaji wa shughuli za mawaziri hao katika maeneo yao.”
Chanzo. VOA
No comments:
Post a Comment