Social Icons

Friday, 20 September 2013

MENGI V/S PROFESA MUHONGO NA MASLAHI YA UMMA.



WIKI iliyopita nilisisimshwa na mjadala mitandaoni, kwenye vyombo vya habari, na hata mitaani kuhusu malumbano  kati ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na mmiliki wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuhusu suala la vitalu vya madini na gesi asilia.

Msisimko huo umenisukuma kuchangia katika mjadala huo kupitia safu hii. Nimeshawishika kuchangia kwa sababu mbili kubwa. Kwanza, ni ukweli kuwa suala la madini na gesi linatuhusu sote kama taifa, na hivyo ni wajibu wetu sote kupima kama malumbano ya wawili hao yanalenga maslahi mapana zaidi ya taifa.

Lakini pili, nimeshawishika kuchangia kwa sababu ya imani yangu kuwa haya si malumbano kati ya Mengi na Muhongo tu; bali ni kati ya wafanyabiashara wazawa wanaowakilishwa na Mengi  dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete inayowakilishwa na Waziri Muhongo. Kwa hiyo, hili ni suala kubwa kuliko tunavyofikiria.

Labda nianze na ya Mengi. Katika taarifa yake ndefu ya majibu yake kwa Muhongo iliyosambazwa mitandaoni na kuchapishwa magazetini, wiki iliyopita, alimtuhumu Profesa Muhongo kwa kusambaza sms inayomchafua inayosomeka hivi:

“Ambieni Watanzania kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752. Amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. Watanzania wanakosa mapato na ajira. Sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je, huu ndiyo uzawa?”

Hivyo ndivyo Mengi alivyouanza utetezi wake; yaani alianza (para ya pili tu) na nukuu hiyo ya sms ya Muhongo. Hiyo maana yake ni kuwa, hilo ndilo jambo lililomkasirisha kuliko mengine yote yaliyozungumzwa dhidi yake na Mulongo.

Hata hivyo, kwa mshangao wangu, Mengi alikwepa kuzungumzia tuhuma hizo katika taarifa yake hiyo ndefu ya utetezi aliyoipa kichwa kinachosomeka: Majibu ya Reginald Mengi juu ya gesi.

Yaani aliishia tu kusema; “huo ni upotoshwaji wenye lengo la kututoa kwenye hoja ya msingi ya raslimali yetu ya gesi. Sijawahi kufanya udalali kwenye vitalu vya madini. Huo ni uongo wa hali ya juu.”

Mtu unaweza kushawishika kuamini kuwa Mengi hajafanya udalali wowote kwenye vitalu vya madini, na hana nia hiyo, lakini vipi dai jingine kuu la Profesa Muhongo kwamba yeye (Mengi) anashikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752 kwa muda mrefu bila kuviendeleza?

Mbona hilo Mengi hakulitolea ufafanuzi kwenye taarifa yake ndefu? Je, ni kweli kuwa anashikilia vitalu vyote hivyo kwa muda mrefu bila kuviendeleza?

Nauliza hivyo kwa sababu, kama ni kweli, basi hoja yake kuwa Muhongo anakwepa hoja ya msingi ambayo ni gesi asilia, haina mantiki. Madini na gesi asilia vyote ni raslimali za nchi, na kwa maana hiyo, umma una haki ya kujua ukweli wa vyote viwili.

Jambo jingine linalonishangaza katika utetezi wa Mengi kwenye taarifa yake hiyo, ni pale anapokaa pia kimya kuzungumzia tuhuma nyingine ya Muhongo kwamba, baada ya kumiliki vitalu vingi vya madini kwa muda mrefu bila kuviendeleza, sasa anataka pia kumiliki vitalu vya gesi asilia.

Kwa kutogusia kabisa dai hilo katika majibu yake, Mengi ameuacha umma na swali moja kubwa; je, ni kweli kwamba anataka pia kumiliki vitalu vya gesi asilia?

Kwa mtazamo wangu, Swali hilo ni muhimu kwa sababu, kama ni kweli anataka kumiliki pia vitalu vya gesi; ilhali amekuwa akimiliki vitalu vingi vya madini kwa muda mrefu bila kuviendeleza, basi, Profesa Muhongo anaweza akawa na hoja nzito dhidi yake.

Isitoshe, kama ni kweli kuwa pia anataka kumiliki vitalu vya gesi asilia, basi utetezi wake ule wa mwanzo kuwa tuhuma ambazo Profesa Muhongo anamrushia zinalenga katika kuwatoa Watanzania kwenye hoja ya msingi ya raslimali yetu ya gesi, unakosa mashiko.

Nasema hivyo kwa sababu, kama nilivyoeleza mwanzo, inapotokea ‘wateule’ kwenye suala la vitalu vya madini ndiyo hao hao wanaowania pia vitalu vya gesi asilia, basi, masuala hayo yanahusiana moja kwa moja, na hivyo kulijadili moja si mbinu ya kukwepa jingine kama Mengi anavyodai.

Vyovyote vile, mtazamo wangu mimi ni kwamba, si haki kwa mwekezaji yeyote mmoja (awe mzawa au mgeni) kumilikishwa vitalu vingi vya madini na kukaa navyo muda mrefu bila kuviendeleza; ilhali wengine wenye uwezo wa kuviendeleza wanavitafuta na hawavipati.

Kwa maana hiyo, naunga mkono msimamo wa Serikali ya Kikwete wa kufuta leseni za makampuni 102 yaliyogaiwa vitalu vya madini kwa muda mrefu bila kuviendeleza.

Na kwa hakika, matarajio yangu ni kwamba hatua hiyo pia itaigusa raslimali ardhi ambako vigogo kadhaa nchini (kama Frederick Sumaye, Mohamed Enterprises nk) wanashikilia, kwa miaka mingi, maelfu ya hekta za ardhi bila kuziendeleza; ilhali wanavijiji yaliko mashamba hayo  hawana ardhi ya kutosha ya kulima.

Kwa ufupi,  jamii inayoruhusu watu wachache kumiliki sehemu kubwa ya raslimali za taifa bila kuziendeleza; ilhali wananchi walio wengi hawana kitu kabisa, ni jamii inayokaribisha umwagaji damu. Na dalili za umwagaji damu nimeshaziona sehemu kadhaa nchini nilizozitembelea nikiwa na ujumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kujionea ukubwa wa tatizo la migogoro ya ardhi.

Ni matumaini yangu, hivyo basi, kwamba wizara ya Profesa Muhongo itakapofuta vibali hivyo vya kumiliki vitalu vya madini, itavigawa upya kwa watu wengi zaidi badala ya kuwalundikia watu wachache vitalu vyote. Ni matumaini yangu vilevile kwamba, wachimbaji wadogo wadogo watapewa kipaumbele katika ugawaji huo mpya.

Hayo pembeni, nikirejea kwa ya Profesa Muhongo, namuunga mkono Mengi kwamba waziri huyu ameonyesha ukigeugeu mkubwa katika suala la ugawaji wa vitalu vya gesi.

Mara alipoingia madarakani, waziri huyu alitusisimsha sana baadhi yetu alipoliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kusimamisha kwanza ugawaji wa vitalu vya gesi asilia mpaka hapo taifa litakapokuwa na sera ya taifa ya gesi asilia. Kwa hakika, alitukosha zaidi alipoliagiza pia TPDC kupitia upya mikataba yote ya gesi asilia.

Kwa kuzingatia kuwa gesi asilia katika Tanzania ni kitu kipya, na kwamba hatuna uzoefu nacho, wengi tulimuunga mkono Profesa Muhongo kwa hatua yake hiyo. Tulimuunga mkono kwa sababu tuliona kuwa ni sahihi kwa taifa kuandaa kwanza sera kuhusu jambo hilo kabla ya kugawa vitalu kwa wawekezaji. Na hivyo ndivyo Profesa Muhongo alivyouahidi umma Septemba 2012.

Sasa, kama anavyoshangaa Mengi, ndivyo pia wengi wetu tunavyoshangaa; inakuaje msomi huyu aliyebobea katika fani ya jiolojia abadilike haraka hivyo katika kipindi kifupi tu? Je, hiyo kweli ndiyo hulka ya msomi aliyebobea?

Lakini hata kama hilo utaliweka pembeni, je; inaingia akilini mwako kuwa ni busara kugawa kwanza vitalu vya gesi asilia, na kisha baadaye ndiyo utoe sera? Nionavyo (na tuko wengi), sera kwanza, na kisha ugawaji vitalu baadaye.

Nini kimembadilisha ghafla Profesa Muhongo kiasi cha sasa kutanguliza kwanza ugawaji badala ya sera, ni kitu kinachosumbua vichwa vya wengi. Ni maoni yangu kwamba kuna kilichojificha nyuma ya kubadilika kwake huko kwa haraka.

Nasema hivyo; maana hata utetezi wake kwamba eti lazima tuharakishe kugawa vitalu vya gesi asilia kwa sababu tunashindana na Msumbiji, haina busara yoyote ndani yake. Hivi kweli taifa lifanye mambo ya haraka haraka na ya hovyo hovyo kwa sababu tu tunataka kushindana na jirani zetu? Lojiki ya ajabu hiyo!

Ndiyo maana katika hilo, namuunga Mengi mkono kwamba, lojiki ni kwanza kuandaa sera ya taifa ya gesi asilia, na kisha ugawaji wa vitalu utafuata baadaye.

Kama watawala wetu wana haraka zao za kugawa vitalu hivyo, basi nawauharakishe mchakato wa kutoa sera ya taifa ya gesi asilia badala ya kukimbilia kuharakisha ugawaji wa vitalu.

Kwa haraka hiyo wanayoionyesha ya kugawa vitalu vya gesi asilia bila kwanza kuwa na sera ya taifa, na kwa kumbukumbu tulizonazo za mgodi wa Buzwagi ambao mkataba wake ulisainiwa kifisadi usiku huko London, kwa nini tusiamini kuwa kuna ajenda iliyojificha kwenye suala hili la ugawaji vitalu vya gesi asilia, na ajenda hiyo yaweza kuwa ya kifisadi?

Hata hivyo, hisia zangu kuhusu kubadilika huko kwa haraka kwa Profesa Muhongo ni kwamba nyuma yake lipo shinikizo la wakubwa wanaotaka kujimilikisha haraka (au jamaa zao) baadhi ya vitalu vya gesi asilia kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015!

Si imebaki miaka miwili tu na ushee muda wao wa kuwa madarakani uishe, na hivyo ni kipindi cha sanya sanya za lala salama?! Ukikumbuka ya miaka ya mwisho ya utawala wa Mkapa, hutashangazwa na hilo.

Na kwa sababu ya hisia zangu hizo, nilitaraji Profesa Muhongo angejiuzulu uwaziri badala ya kukubali kushinikizwa kugawa vitalu vya gesi asilia kabla ya taifa kuwa kwanza na sera kuhusu raslimali hiyo – kitu ambacho aliuahidi umma Septemba 2012.

Vyovyote vile, kukubali kwake  haraka ‘kumeza matapishi yake’ (turn about) katika suala hili la vitalu vya gesi asilia, kumempunguzia heshima; maana sasa haonekani tena kama ni mtu wa misimamo.

Nihitimishe kwa kusisitiza tena kwamba namuunga mkono Mengi kuwa raslimali za Tanzania zinapaswa kuwanufaisha zaidi Watanzania badala ya kuwanufaisha zaidi wageni. Lakini hiyo haihalalishi kumlundikia mzawa mmoja vitalu vingi bila kuviendeleza. Huo ni u-mimi na ulafi wa kibepari ambao hauifai jamii yetu!

Kwa hakika, kama ingekuwa ni utashi wangu ningeweka sera na sheria zinazohakikisha kwamba asilimia 70 ya vitalu vya gesi asilia nchini vinamilikiwa na Watanzania wote kupitia shirika lao la umma la TPDC ili hao wawekezaji wageni na wazawa wagombee asilimia 30 zinazobakia!

Ndugu zangu, hivyo ndivyo wafanyavyo kwingineko kwenye tawala makini. Hata Russia ambako kuna utawala wa kibabe wa Rais Putin, kampuni kubwa kushinda zote za mafuta na gesi katika nchi hiyo na barani Ulaya inayoitwa Rosneft inamilikiwa na serikali kwa asilimia 75; huku kampuni ya Uingereza ya BP ikiambulia asilimia 19 tu!

Nasi, tukitaka, twaweza kufanya hivyo hivyo kwa TPDC yetu. Na hilo lingepunguza malumbano haya ya sasa ya kina Mengi na Profesa Muhongo wetu ambayo, kwa mtazamo wangu, hayalengi katika maslahi mapana zaidi na ya muda mrefu ya taifa letu bali utajirisho wa watu wachache , na hasa vigogo.


Chanzo :- Raia Mwema


No comments:

 
 
Blogger Templates