MTANDAO wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), umesema hali ya wananchi wa Mtwara si nzuri kwa vile wanaishi kwa shaka kubwa na wameathirika kisaikolojia kutokana na suala la mradi wa gesi. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Bebron Mwakagenda alisema hilo limebainika baada ya mtandao huo kutembelea mkoa huo na kufanya utafiti.
Wanachama 30 wa TCDD kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Mara, Kigoma, Mwanza, Pwani na Dar es Salaam walihusika katika utafiti huo, alisema.
Mwakagenda alisema tangu kutokea vurugu zilizotokana na mradi wa gesi katika Manispaa ya Mikindani amani haipo na waandishi wa habari wa mkoa huo wamezuiwa kuandika habari zinazohusu mkoa huo hadi zithibitishwe na baadhi ya viongozi.
Alisema utafiti wao umebaini watu waliohusika kuchangia vurugu zilizosababisha mali za watu kuharibiwa, watu kupigwa na wengine kuuawa ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikuwa akitoa kauli za kuwakebehi wananchi.
Wengine waliochangia kuibuka vurugu ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara (RPC), Linus Sinzumwa na Mkuu wa Mkoa huo, Joseph Simbakalia ambao wote kwa pamoja waliwazuia wananchi kujieleza kwa njia ya maandamano ambayo ni haki yao ya msingi, alisema.
Alisema mambo mengine yaliyobainika kwenye uchunguzi huo ni kiwanda cha saruji kilichoahidiwa kujengwa na tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote hadi sasa hakijajengwa na hakuna dalili za ujenzi huo huanza.
“Hata hivyo tumaini lililoonekana kwa wananchi hao ni kumtaka Rais Jakaya Kikwete aende katika mkoa huo azungumze nao uwanjani ili kutibu majeraha waliyonayo yaliyotokana na mradi wa gesi,” alisema.
Chanzo:- Mtanzania.
No comments:
Post a Comment