Urusi imelipigia kura ya turufu azimio linaloungwa mkono na mataifa ya magharibi lenye kulaani kura ya maoni ya Crimea katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi(15.03.2014).
Rasimu ya azimio hilo lenye kusema kura hiyo ya maoni ya Jumapili haitokuwa na maana imeungwa mkono na kura 13 katika Baraza la Usalama la nchi wanachama 15 lakini limekataliwa wakati Urusi mwanachama wa kudumu wa baraza hilo ilipotumia kura yake ya turufu kulizuwiya. China mwanachama mwengine wa kudumu wa baraza hilo haikushiriki katika kupiga kura hiyo na kuifanya Urusi izidi kutengwa katika suala la mzozo wa Ukraine.
China ambayo mara nyingi imekuwa ikiiunga mkono Urusi katika baraza hilo hususan katika kura kuhusiana na masuala ya Syria,wanadiplomasia wameiona hatua yake ya kujitowa kupiga kura ni matokeo mazuri ambayo yangeliweza kupatikana katika kura hiyo ya leo.
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Liu Jieyi amesema kupitisha azimio kuhusu Ukraine wakati huu kutakuja tu kusababisha malumbano na kuifanya hali hiyo kuzidi kuwa ngumu.
Balozi wa Marekani Samantha Power ameliambia baraza hilo katika kikao chake cha saba cha dharura kuhusu Ukraine tokea kuanza kwa mzozo wa nchi hiyo kwamba Urusi iliotengwa, ilioko peke yake na inayofanya makosa imekwamisha kupitishwa kwa azimio hilo.
Ameongeza kusema katika hotuba yake fupi "Hivi tunavyozungumza vikosi vya ulinzi vya Urusi vinakusanyika kwenye mpaka wa mashariki na Ukraine."
Kerry, Lavrov washindwa kupata muafaka
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, na mwenzake wa Marekani, John Kerry, wameshindwa kutatua tofauti zao juu ya mkoa huo wa Crimea, hata baada ya mazungumzo yao ya masaa nyumbani kwa balozi wa Urusi nchini Uingereza hapo jana (tarehe 14 Machi 2014).
Wakizungumza kwa pamoja na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao, mawaziri hao walionesha wazi kutokufikia makubaliano yoyote katika suala hilo tete linalozidi kuzigawa serikali zao, licha ya wote kusema kuwa yalikuwa mazungumzo ya kuridhisha.
Hata hivyo, Lavrov alirejelea msimamo wa nchi yake kwamba haina nia ya kuingilia kijeshi nchini Ukraine, ingawa hakuonesha uwezekano wowote wa pande hizo mbili kuwa na msimamo wa pamoja juu ya hali ya mambo kwenye mkoa wa Crimea.
Kwa upande wake, Kerry alisema baada ya mazungumzo hayo marefu, mwenzake Lavrov aliweka wazi kwamba "Rais Putin hayuko tayari kuamua chochote juu ya Crimea hadi kura ya maoni itakapofanyika", akiongeza kwamba msimamo wa Marekani juu ya kura hiyo ya maoni unabakia kuwa ule ule kuwa "inakiuka katiba ya Ukraine, na sheria za kimataifa na tunaamini si halali."
Kwa mara nyengine, Lavrov alizionya nchi za Magharibi dhidi ya kuiwekea nchi yake vikwazo vya kidiplomasia au vya kiuchumi kutokana na msimamo wake juu ya Ukraine. Wakaazi wa Crimea watapiga kura ya maoni ya ama kujiunga na Urusi au kuwa taifa huru hapo kesho, baada ya bunge la mkoa huo kuamua wiki iliyopita kujiunga na Urusi. Kesho hiyo hiyo pia, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wataamua hapo kesho juu ya orodha ya Warusi watakaolengwa na vikwazo hivyo.
Marekani yawaonya raia wake
Waungaji mkono wa Ukraine katika mji wa Simferopol, Crimea, wakipinga kura ya maoni ya kuamua ikiwa mkoa huo ujiunge na Urusi ama la.
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaonya raia wake juu ya uwezekano wa mapambano ya kijeshi kwenye mpaka wa Ukraine na Urusi na pia vuguvugu la kuipinga Marekani nchini Urusi, huku Crimea ikijiandaa na kura hiyo ya kujiunga na Urusi.
Licha ya kusema kwamba haina taarifa yoyote ya mgogoro wa kijeshi ndani ya Urusi kutokana na wasiwasi uliopo kwenye eneo hilo au kitisho chochote kwa raia wake, Marekani imesema kupitia "onyo la safari" kwamba raia wake walio kwenye eneo hilo na wale wanaopanga kwenye huko wanapaswa kuwa na tahadhari.
Katika kile kinachoonekana kama makabiliano mabaya kabisa tangu kuanza wakati wa Vita Baridi, Urusi ilituma wanajeshi zaidi mkoani Crimea siku ya Ijumaa na kutishia kupeleka wanajeshi kwenye maeneo mengine ya Ukraine kufuatia ghasia zilizotokea usiku wa Alhamis kwenye mkoa wa Donetsk.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Amina Abubakar
Chanzo:- dw.de
No comments:
Post a Comment