Social Icons

Saturday, 15 March 2014

Baraza la Usalama kupiga kura juu ya Ukraine

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kwa dharura kulipigia kura azimio dhidi ya kura ya maoni mkoani Crimea linaloungwa mkono na Magharibi, huku Marekani na Urusi zikishindwa kukubaliana juu ya Ukraine.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York.

Kikao hicho cha dharura ambacho kinapangwa kuanza saa 5:00 asubuhi kwa saa za New York hivi leo (tarehe 15 Machi 2014), kimeitishwa kwa ombi la serikali ya Marekani. Wanadiplomasia wanasema wanatarajia Urusi kulipigia kura ya veto azimio hilo, lakini bado haijafahamika ikiwa China nayo itafanya hivyo hivyo au la.

Kawaida Urusi na China huwa na msimamo mmoja kwenye Baraza hilo la Usalama, hasa kuhusiana na suala la Syria. Chanzo chengine cha kidiplomasia kimesema kuwa lengo pekee la azimio hilo ni kuifanya China ijizuwie kupiga kura na hivyo kuitenga zaidi Urusi.

Inasemekana kuwa azimio hilo limeandikwa kwa lugha ambayo itaishawishi China, kwani haliitaji moja kwa moja Urusi, halitishii vikwazo na wala kuitaka Urusi kuondoa wanajeshi wake mkoani Crimea, ambako kawaida imekuwa na kituo cha kijeshi. Msimamo wa China umekuwa ni kuheshimu uhuru na mamlaka ya taifa na kujizuia kuingilia mambo ya ndani ya nchi husika.

Kerry, Lavrov washindwa kupata muafaka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov (kushoto) na mwenzake wa Marekani, John Kerry.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov (kushoto) na mwenzake wa Marekani, John Kerry.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, na mwenzake wa Marekani, John Kerry, wameshindwa kutatua tofauti zao juu ya mkoa huo wa Crimea, hata baada ya mazungumzo yao ya masaa nyumbani kwa balozi wa Urusi nchini Uingereza hapo jana (tarehe 14 Machi 2014).

Wakizungumza kwa pamoja na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao, mawaziri hao walionesha wazi kutokufikia makubaliano yoyote katika suala hilo tete linalozidi kuzigawa serikali zao, licha ya wote kusema kuwa yalikuwa mazungumzo ya kuridhisha.

Hata hivyo, Lavrov alirejelea msimamo wa nchi yake kwamba haina nia ya kuingilia kijeshi nchini Ukraine, ingawa hakuonesha uwezekano wowote wa pande hizo mbili kuwa na msimamo wa pamoja juu ya hali ya mambo kwenye mkoa wa Crimea.

Kwa upande wake, Kerry alisema baada ya mazungumzo hayo marefu, mwenzake Lavrov aliweka wazi kwamba "Rais Putin hayuko tayari kuamua chochote juu ya Crimea hadi kura ya maoni itakapofanyika", akiongeza kwamba msimamo wa Marekani juu ya kura hiyo ya maoni unabakia kuwa ule ule kuwa "inakiuka katiba ya Ukraine, na sheria za kimataifa na tunaamini si halali."

Kwa mara nyengine, Lavrov alizionya nchi za Magharibi dhidi ya kuiwekea nchi yake vikwazo vya kidiplomasia au vya kiuchumi kutokana na msimamo wake juu ya Ukraine. Wakaazi wa Crimea watapiga kura ya maoni ya ama kujiunga na Urusi au kuwa taifa huru hapo kesho, baada ya bunge la mkoa huo kuamua wiki iliyopita kujiunga na Urusi. Kesho hiyo hiyo pia, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wataamua hapo kesho juu ya orodha ya Warusi watakaolengwa na vikwazo hivyo.

Marekani yawaonya raia wake

Waungaji mkono wa Ukraine katika mji wa Simferopol, Crimea, wakipinga kura ya maoni ya kuamua ikiwa mkoa huo ujiunge na Urusi ama la.

Waungaji mkono wa Ukraine katika mji wa Simferopol, Crimea, wakipinga kura ya maoni ya kuamua ikiwa mkoa huo ujiunge na Urusi ama la.

Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaonya raia wake juu ya uwezekano wa mapambano ya kijeshi kwenye mpaka wa Ukraine na Urusi na pia vuguvugu la kuipinga Marekani nchini Urusi, huku Crimea ikijiandaa na kura hiyo ya kujiunga na Urusi.

Licha ya kusema kwamba haina taarifa yoyote ya mgogoro wa kijeshi ndani ya Urusi kutokana na wasiwasi uliopo kwenye eneo hilo au kitisho chochote kwa raia wake, Marekani imesema kupitia "onyo la safari" kwamba raia wake walio kwenye eneo hilo na wale wanaopanga kwenye huko wanapaswa kuwa na tahadhari.

Katika kile kinachoonekana kama makabiliano mabaya kabisa tangu kuanza wakati wa Vita Baridi, Urusi ilituma wanajeshi zaidi mkoani Crimea siku ya Ijumaa na kutishia kupeleka wanajeshi kwenye maeneo mengine ya Ukraine kufuatia ghasia zilizotokea usiku wa Alhamis kwenye mkoa wa Donetsk.

Chanzo:- dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates