Serikali imeanza kujenga Uwanja wa Michezo Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 8.2 utaomilikiwa na Halmashuri ya Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro amesema uwanja huo utakuwa na viwanja vitano vya michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwanja wa mpira wa miguu,riadha,mpira wa pete,mpira wa wavu na mpira wa kikapu.
Kinawiro amesema hivi sasa waeunda kamati ya uhamasishaji wa ujenzi inayoongozwa na Aidan Msigwa na mpaka sasa wamefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 56 na wameanza kufyatua tofari za saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa maduka kuzunguka uwanja huo.
Aidha kapuni ya saruji ya Mbeya(LAFARGE) wametoa mifuko 500 ya saruji kuunga mkono juhudi za serikali wakati kampuni ya ujenzi wa Barabara kati ya Lwanjilo/Chunya wao watagharamia kuutengeneza uwanja wa mpira wa miguu kwa kupanda nyasi na uwekaji wa magoli.
Mkuu wa wilaya amesema fursa iko wazi kwa watu watakaokuwa tayari kujenga viwanja vilivyosalia na mchango wao watauthamini na kuuweka kwenye kumbukumbu na makampuni hayo yatatumia uwanja huo kujitangaza kibiashara.
Amesema ni wakati mzuri kwa makampuni hayo kuwekeza katika sekta ya michezo hivyo kuyataka makampuni yaliyoko wilayani Chunya na kwingineko kuitumia vema fursa hiyo kama vile makampuni ya madini,vinywaji na makampuni ya simu za mikononi.
Hata hivyo Kinawiro amewataka wananchi kila mmoja ashiriki kutoa mchango kwani mbali ya kuwa kitega uchumi cha Halmashauri pia utatoa ajira kwa wakazi wa wilaya ya Chunya hivyo kuondoa tatizo la ajira kwa vijana na kuwafanya vijana kuimarisha afya zao kwa kushiriki michezo mbalimbali kwa viwanja vitakavyojengwa.
Wilaya ya Chunya imeanza kukua kwa kasi baada ya Serikali kuanza ujenzi wa barabara ya Mbeya/Chunya hali inayowafanya wawekezaji kuanza kuelekeza nguvu zao huko na kutoa fursa kwa wakazi hao kukuza pato kwa wananchi.
Na Mbeya yetu |
No comments:
Post a Comment