Social Icons

Wednesday 24 September 2014

HADITHI: Missed call ya shemeji -21


“Hapokei?” aliuliza Ummy kwa sauti ya chini kidogo kwani bado alikuwa hana raha.
“Hapokei,” alijibu Aisha, akapiga tena…
Mara Salma alitokea akiwa kasi ameshika simu ya Ummy…
“Simu yako inaita bosi,” alisema Salma huku akimkabidhi.
JIRUSHE MWENYEWE…

Ummy aliiweka simu aliyotoka nayo ndani kwenye mapaja, akaipokea aliyoletewa na Salma ambayo ilikuwa ikipigwa na Aisha wakiwa wote pale.Ummy alihisi kuumbuka kwani simu aliyoletewa ndiyo aliyokuwa akichati na Aisha.

Alijifanya anaipokea,  lakini akaikata huku akiendelea kuongea…
“Haloo, niambie mama Eliza, hajambo Eliza? Sisi tupo bwana, tunaendelea na kazi tu, sijui wewe. Haya…sawa nimekuelewa mama Eliza.”

Alipomaliza alimwangalia Aisha na kumuuliza…
“Vipi, umempata?”
“Mh! Mtu mwenyewe amekata simu bwana,” alisema Aisha huku akimwangalia Ummy kwa macho yenye kuomba msaada.

“Atakuwa amekuona hapo nje akaingia mitini, si ajabu alitaka kutumia jina la benki yetu kufanya utapeli kwamba anafanyia hapa, sisi hatuna mfanyakazi huyo,” alisema Ummy.
Baada ya kuongea hayo, ulipita ukimya mkubwa, hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzake, si Aisha si Ummy. Walipomaliza vinywaji, Aisha aliaga kuondoka ambapo muda mrefu Ummy alitamani aondoke ili ajue moja.

“Basi sawa, mimi naondoka Ummy.”
“Sawa, lini upo nyumbani nije kukutembelea?”
“Mmmh! Wikienda huwa sitokagi, karibu sana.”
“Oke, basi nitakupigia kwanza kabla sijaja.”
“Sawa.”

Ummy akiwa anarudi ofisini alimpigia simu Beka…
“Baby…”
“Yes baby,” aliitika Beka akiwa hajui hili wala lile…
“Unajua mkeo leo alikuja ofisini kwangu…”
“Mke wangu alikuja ofisini kwako?”
“Ndiyo baby.”

“Kufanya nini na umemjuaje kuwa ni yeye?”
“Mh! We acha tu! Ni stori ndefu sana.”
Ummy alimsimulia kila kitu Beka. Beka naye akaanza kuumiza kichwa kwamba, mkewe aliipata wapi namba ya simu ya Faidha. Pia Beka mwenyewe alikuwa hajui kama Faidha ana jina jingine la Ummy.
“Mh! Labda alichukuwa namba yako kwenye simu yangu asubuhi.”
“Labda, mimi nilishindwa kumuuliza namba yangu aliipata wapi!”

* * *
Aisha naye aliendelea kuumiza kichwa kuhusu huyo Faidha, kwamba ni kweli alikuwa akimtapeli kufanya kazi pale benki au yupo lakini kafichwa?
Alipofika nyumbani jioni alikaa sebuleni, akachukuwa laptop yake na kuingia kwenye Facebook, akaandika jina Faidha.

“Mh!” aliguna Aisha kwani picha iliyojitokeza hapo ni ya Ummy…
“Mungu wangu, naona kweli au nipo usingizini naota?  Faidha ni Ummy?” alisema Aisha.
Akaendelea kupekuwa Facebook hiyo ambapo pia Faidha alijiandika kwamba hana mume jambo ambalo Aisha alilikubali maana alimwambia anatoka na mume wa mtu, aliandika pia anafanya kazi kwenye benki hiyo.

“Ni yeye,” alisema akikiri moyoni mwenyewe. Aliendelea kuangalia mambo mbalimbali kwenye Facebook hiyo ambapo alikutana na mambo yaliyompa ushahidi wa moja kwa moja kwamba, kweli yule ni Faidha ana uhusiano na mume wake, mfano alikutana na posti ya Ummy ikiwa imeandikwa hivi:
“Kama unajitambua kuwa ni mke, mpe haki yake mumeo na mheshimu sana ukimtii kwa kila jambo, ukilegea hapo unaweza kunyang’anywa ukabaki na kilio kama akina f’lani.”
Pia alikutana na posti nyingine ikiwa na maneno haya…

“Ni aibu kweli, mke anamkatalia mumewe tendo la ndoa, akitoka nje mume watampapatikia, we ulie tu.”

“Huyu ni yeye, haya maneno pia yamenilenga mimi, lazima,” alisema moyoni Aisha akiumia. Aliangalia juu kwa muda akifikiri cha kufanya, akapata wazo la kumpigia simu Ummy kumweleza uovu wake…
“Haloo Ummy,” aliita Aisha baada ya Ummy kupokea…
“Niambie Aisha, upo nyumbani?”

“Nipo, Ummy namshukuru sana Mungu nimemjua Faidha ni nani!”
“Ni nani?” Ummy aliuliza kwa haraka sana.
“Si wewe.”
“Mimi?”
“Ni wewe ndiyo.”
“Kivipi?”

“Nipo Facebook hapa, naona picha yako, tena umeweka wazi unakofanyia kazi ndiyo hapo nilipokuja ukasema humjui, loo! Ummy, yaani unanichukulia mume hivihivi naona?”
“Khaa! Aisha, mbona sikuelewi?”
“Umeshanielewa, acha hizo bwana.”

Ummy alichoona mbele yake ni kukata simu haraka sana kisha akaizima kabisa huku akisonya chini kwa chini lakini moyoni alisema...
“Du! Nimeumbuka. Kweli picha ya kwenye Facebook imeniumbua, hilo halina ubishi hata kidogo. Sasa?” alikosa majibu.

Kwa upande wake, Aisha baada ya kukatiwa simu na Ummy au Faidha, alimwandikia meseji…
“Kata simu, kataa niliyosema lakini ukweli ni kwamba wewe Faidha unatembea na mume wangu, Beka.”
Akaituma akisubiri idelive wakati wowote.

* * *
Faidha alichukuwa simu nyingine na kumpigia simu Beka…
“Dear mambo yamemwagika huku…”
“Yamemwagikaje?”
“Mkeo si nilikwambia mpaka pale tulipoachana?”
“Ndiyo. Imekuaje?”

Inaendelea 

Chanzo globalpublishers 


1 comment:

Basahama said...

Tumeikubali HADITHI hiii

 
 
Blogger Templates