“Kwani pete yake si anayo?” dada yake Hailat aliuliza.
“Ndiyo lakini nashangaa simuoni.”
“Basi atakuwa ameivua.”
“Hebu rudi kwanza ndani ukaangalie vizuri,” mama yake alimshauri.
Nargis alirudi ndani kuangalia tena, lakini alikuta hali ni ileile kiza kizito kilitanda eneo lile.
SASA ENDELEA...
Alitoka kwenda kuwaeleza nao walinyanyuka na kuingia naye chumbani kwake kuangalia. Walishtuka kuona kiza kizito sehemu iliyokuwa ikimuwezesha Nargis kumuona mumewe.
“Mmh! Itakuwa nini?” Dada yake Hailat alishtuka.
“Mmh! Lazima kuna mchezo umechezwa si bure,” mama yake alijibu.“Kibaya hata sioni dalili za pete,”Nargis alisema kwa kukata tamaa.
“Siyo tatizo, watume Watwana wakamtie uchovu akirudi nyumbani wamvue pete na kuileta huku na kuirudishia nguvu yake kisha tutamchukua na kumwekea kivuli kisha tunamrudisha duniani huku tukiwaondoa wafanyakazi wote wanadamu na kampuni yake itaendeshwa na majini, kila atakapokuwa wanadamu hawatamuona,” alisema mama yake.
“Hilo ndilo la kufanya japokuwa najua vita ya wanadamu ni nzito sana, basi tu mdogo wangu mbishi kwa nini usiachane na huyo mwanaume kwa vile tayari amekupatia watoto,” dada yake alimshauri.
“Dada hayo ni maneno gani? Kumbuka yule ni mume wangu wa ndoa halali, baba wa watoto wangu, siwezi kurudi nyuma nitapambana hadi tone la mwisho la damu yangu,” Nargis alisema kwa uchungu.
“Basi tu ingekuwa amri yangu ningemuulia mbali mwanaume anayekosa uaminifu,” dada yake alisema kwa hasira.
“Mmh! Sasa hebu waite watwana wafanye hiyo kazi muda huu,” Malkia Zabeda alitoa amri.
Nargis alijishika katika paji la uso, mara walitokea watwana na kupiga magoti mbele yake na kuuliza.
“Mwana wa mfalme una shida gani?”
Aliwapa maelekezo ya kumtia uchovu Thabit, akilala wachukue ile pete haraka na kuipeleka chini ya bahari. Baada ya kuelezwa vile walitoweka ghafla na kwenda moja kwa moja ndani ya ofisi alipokuwa Thabit amerudi muda mfupi toka hotelini walipokwenda kupata chakula cha mchana na Subira.
Waliingia na kumpuliza kisha walisimama pembeni, ghafla Thabit alianza kujinyoosha baada ya kusikia uchovu mkubwa mwilini mwake. Aliona hawezi kuendelea na kazi alitoka na kumuaga Subira aliyeshtuka na kurudi nyumbani kulala. Alipopanda kitandani usingizi mzito ulimchukua.
Watwana waliotumwa walimvua pete na kuondoka nayo kurudi nayo chini ya bahari, walipofika walimkabidhi Nargis. Aliipokea na kuishangaa ilivyokuwa imepoteza mvuto kwani ilikuwa imechakaa sana. Hakuamini kama ile ndiyo pete aliyomvalisha mumewe Thabit.
Baada ya kuichunguza sana aligundua ilikuwa yenyewe isipokuwa ilichezewa na kuondolewa nguvu za kijini. Baada ya kugundua hali ile roho ilimuuma sana mpaka machozi yakamtoka. Moyoni alijikuta akiwachukia wanadamu kwa kitendo cha kumchokonoa kila kukicha.
Aliishika ile pete na kumpelekea mama yake huku akilia.
“Mama hebu ona jinsi wanadamu wanavyonitafuta ubaya.”
“Mmh! Kazi ipo kama pete imekuwa hivi basi kweli wamefanya kazi kubwa.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Irudishiwe nguvu, irudishwe kwa Thabit kisha aletwe hapa mara moja.”
Ilichukuliwa pete na kurudishiwa nguvu kubwa kuliko ya awali ambayo kila atakayeigusa kwa nia mbaya anaungua moto.
Pete ilikuwa ikiwaka mwanga mkali, kama una nia mbaya ukiutazama lazima ukupofue macho.
Pete ilikuwa nzito kubebeka hata Nargis ilimshinda kuinyanyua na kumuuliza mama yake.
“Mama mbona imekuwa nzito hivi?”
“Uzito wake ndiyo utakavyokuwa uzito wa mumeo, hataguswa na kitu chochote.”
“Sasa ataivaaje?’
“Hebu ibebe tena.”
Nargis alibeba na kushangaa kuona ikiwa nyepesi kama kawaida:
“Mbona imekuwa nyepesi?”
“Ilikuwa haijapoa sasa hivi ukimvisha mumeo hataguswa na kitu chochote.”
“Asante mama,” Nargis alimshukuru mama yake.
Baada ya zoezi lile waliitwa watwana na kutwa wairudishe pete kwa Thabit na kumchukua kurudi naye chini ya bahari kwa ajili ya kumtengeneza ili asiweze kuonekana kwa macho ya kibinaadamu. Safari ile aliyewaita watwana alikuwa Malkia Zabeda mama wa Nargis ambaye alitoa kauli nzito kuhakikisha hawafanyi mchezo siku zote atakacho watuma na kwenda kinyume ningegharimu maisha yao.
Walipofika kwake walilala kifudifudi ili kusikilia mke wa mfalme anataka kuwatuma nini. Lakini kabla hajawatuma walishtushwa na vilio vya wajakazi walioingia ghafla.
“Kuna nini?” Malkia Zabeda aliuliza kwa mshtuko.
“Hatari, “ walisema kwa pamoja huku wakijilaza kifudifudi mbele na malkia wa bahari.
“Ya nini?”
“Nyumba inawaka moto.”
“Nyumba inawaka moto! Nyumba gani?”
“Ya..ya..dada.”
“Nyumba ya mume wangu Thabit, baba Zumza?” Nargis aliuliza kwa mshtuko.
“Ndi...yo mwana wa mfalme.”
“Mungu wangu!” Nargis alisema huku akishika mikono kichwani.
“Hebu kwanza elezeni vizuri kuna nini?” Hailat dada yake Nargis aliuliza.
“
Tulikuwa ndani tumepumzika, baba Zumza alirudi mapema na siyo kawaida yake na kusema amechoka na kwenda chumbani kwake kupumzika. Ghafla walikuja kina Suunu ambao walisema umewatuma pete ya mumeo. Baada ya kuichukua waliondoka na kutuacha tukimuandalia kinywaji,” alisema mmoja wao.
taendelea
Chanzo Globalpublishers
No comments:
Post a Comment